na Ahmed Makongo, Bunda
SERIKALI imewataka wachimbaji wadogowadogo nchini kujiunga kwenye vikundi pamoja na kuwa na leseni ili serikali iweze kuwatambua na kuwasaidia kujiinua kiuchumi.
Waziri wa Nisahati na Madini Profesa Sospeter Muhongo, aliyasema hayo wilayani Bunda, mkoani Mara, wakati akizungumza na wadau wa umeme, kijiji cha Kibara na mjini Bunda, kwenye mjadala wa kuzungumzia umeme na madini wilayani humo.
Waziri Muhongo alisema kwa kufanya hivyo serikali itawatambua kwa kuwa imetenga sh bilioni 8.9 kwa ajili ya kusaidia wachimbaji wadogo.
Alisema baadhi ya wachimbaji wadogo wadogo hapa nchini wamekuwa wakifanya shughuli hizo bila kuwa na leseni, na kwamba hilo ni kosa la kisheria.
“Kuchimba madini bila kuwa na leseni kisheria ni kosa....ila serikali yenu sikivu imekuwa ikiwaacha tu.....kwa sababu mnajitafutia kipato, hasa ukizingatia kwamba watu wengi hawana kipato, lakini ni vema mkawa na leseni kuepuka kuvunja sheria,” alisema.
Kwa upande wake Meneja wa Madini Kanda ya Ziwa, Salum Salum, alisisitiza ukataji wa leseni kwa wachimbaji hao, na kwamba endapo mtu atavunja sheria faini yake ni sh milioni tano au kifungo cha miaka mitatu jela, au vyote kwa pamoja.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment