Home » » WAZIRI MUHONGO: WEKENI BATI MPATE UMEME

WAZIRI MUHONGO: WEKENI BATI MPATE UMEME

na Ahmed Makongo, Bunda
WAZIRI wa Nisahati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amewataka wananchi wa wilayani Bunda kujenga nyumba bora za bati ili waweze kuwekewa nishati ya umeme.
Prof. Muhongo alitoa rai hiyo jana wakati akiendesha mjadala mkubwa na wadau wa umeme, kuhusu kusambaza nishati hiyo katika vijiji vya Wilaya ya Bunda mkoani Mara.
Mjadala huo uliofanyika maeneo tofauti katika Kijiji cha Kibara na mjini Bunda, ulishirikisha wadau mbalimbali wa umeme kutoka kata zote za majimbo ya Bunda na Mwibara, ambapo Waziri Muhongo alisema wana mpango mkakati wa kufikisha umeme vijijini.
Alisema kuwa kufuatia utekelezaji wa pango huo, wananchi wanapaswa kubadilika na kujenga nyumba bora, ili waweze kuwekewa umeme kwenye nyumba zao, hali ambayo pia itawawezesha kujiletea maendeleo endelevu.
Alisema kuwa katika ufuatiliaji wake ameona nyumba nyingi wilayani hapa zimeezekwa kwa nyasi na kwamba umeme hauwezi kuwekwa kwenye nyumba hizo.
Aidha, alisema kuwa katika bajeti yake wizara hiyo imetenga fedha kwa ajili ya kusambaza umeme vijijini, na kwamba ni vema sasa wananchi wakachangamkia fursa hiyo.
“Katika bajeti ya mwaka huu wizara yangu imetenga fedha kwa ajili ya kusambaza umeme vijijini....sasa umeme hauwezi kuja kwenye nyumba za nyasi, hivyo wananchi jengeni nyumba bora za bati,” alisema.
Alibainisha kuwa TANESCO ilikuwa imetafunwa na wajanja wachache na kwamba sasa wananchi wategemee shirika hilo litarudi kwenye utaratibu wake kama kawaida.
Naye Wakala wa Umeme Vijijini (REA), Mhandisi Bengiel Msofe, alisema kuwa TANESCO katika bajeti ya mwaka huu wa fedha, wamepanga kusambaza umeme kwenye vijiji 33 vya majimbo ya Bunda na Mwibara.
Alivitaja baadhi ya vijiji hivyo kuwa ni Kasuguti, Mahyoro, Kasahunga, Nyamitwebili, Bulamba, Dodoma, Mwitende, Genge, Nambaza, Mwibagi, Bitaraguru, Kihumbu, Mekomariro, Sanzate, Mwitende na Nansimo.
Vingine ni Namibu, Busambara, Salama Kati, Kung’ombe, Kiloreli, Salawe, Kamkenga, Kangetutya, Changunge, Mihingo, Marembeka, Kisangwa, Kabasa, Rwabu, Kunzugu na Nyamatoke.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa