Mwandishi wetu, Bunda.
MKUU wa wilaya ya Bunda Joshua Mirumbe, amewaonya wananchi wanaopeleka habari za uzushi, majungu na uongo kwenye ofisi yake kwa lengo la kutaka kuwachafua viongozi, kwa ajili ya masilahi yao ya kisiasa, kwamba kufanya hivyo ni kosa la jinai.
Mkuu huyo wa wilaya ya Bunda, ametoa tamko hilo wakati akizungumza na Radio Free Africa ofisini kwake mjini Bunda.
Mirumbe amesema kuwa ofisi yake sio ya kuchezea kwa kupeleka taarifa za uongo, uzushi na majungu, kwa lengo la kuchafuana, na kwamba mwananchi yoyote atakayebainika kwa kumpelekea taarifa za uongo ama majungu, atachukuliwa hatua za kisheria kwani hilo ni kosa la jinai.
Hivi karibuni wananchi watano wakazi wa kijiji cha Karukekele wilayani humo, wanadaiwa kughushi sahihi za wananchi wengine wakiwemo walimu wa shule za msingi na kupeleka taarifa ya uongo kwa mkuu huyo wa wilaya, wakilalamikia mwenyekiti wa kijiji hicho, Bw. Jogoro Amoni, kwamba amekula fedha za michango ya wananchi, walizochanga kwa ajili ya ujenzi wa sekondari.
Kufuatia hali hiyo mkuu huyo wa wilaya ya Bunda, alimtuma Ofisa tarafa ya Kenkomyo, Bw. Abiud Jandwa, kufanya uchunguzi wa kina juu ya madai hayo, kupitia vikao halali vya kijiji hicho na ndipo ikabainika kwamba huo ni uzushi mtupu, wenye lengo la kutaka kumchafua mwenyekiti huyo kutokana na masilahi ya kisiasa.
Ofisa tarafa huyo amesema kuwa taratibu za kisheria zinafanyika kwa ajili ya kuwachukulia hatua wananchi hao kwa kutoa taarifa za uongo kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya.
Wakati huo huo mkuu huyo wa wilaya ya Bunda amewataka wananchi wampelekee taarifa ambazo ni sahihi ili achukuwe hatua sitahiki kwa wahusika na kwamba kero zao kwanza zianzie kwa viongozi walioko katika maeneo yao, wakiwemo watendaji wa vijiji, kata na maafisa tarafa, na wanaposhindwa kuzitatua ndipo zipelekwe kwenye ofisi yake.
Blogzamikoa
0 comments:
Post a Comment