Home » » POLISI KUSHITAKIWA MAHAKAMA YA KIMATAIFA

POLISI KUSHITAKIWA MAHAKAMA YA KIMATAIFA

na Ambrose Wantaigwa, Tarime
FAMILIA za wahanga waliouawa mikononi mwa polisi wilayani hapa, wanaandaa utaratibu wa kisheria kuhakikisha Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya, Justus Kamugisha, na watangulizi wake wanafikishwa katika Mahakama ya Kimataifa kwa tuhuma za uhalifu dhidi ya binadamu.
Miongoni mwa madai yao, wamedai askari walioletwa wilayani hapa baada ya kuundwa kanda hiyo, wamekuwa wakiua wananchi wa vijiji vinavyozunguka mgodi wa North Mara kwa madai ya kuuvamia pamoja na ubakaji.
Wakizungumza na Tanzania Daima kwa nyakati tofauti jana, walisema tangu kuundwa kwa kanda hiyo miaka miwili iliyopita, askari wamewapiga risasi ovyo na kuua wananchi zaidi ya 30 kwa kisingizio kuwa wamekuwa wakivamia mgodi huo unaomilikiwa na Kampuni ya African Barrick Gold.
Mmoja wa wananchi hao, Magige Gesabo, alisema kijana wake aliyekuwa akisubiri kujiunga na Chuo Kikuu, Emmanuel Gesabo (27), alikuwa ni miongoni mwa wananchi watano waliopigwa risasi na kuuawa na polisi usiku wa Mei 16, mwaka jana kwa madai ya kushiriki katika uvamizi wa mgodi huo.
Katika tukio hilo, alidai polisi walivamia chumba cha maiti katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime siku mbili baadaye na kupora miili hiyo na kuzuia ibada ya mazishi iliyokuwa imeandaliwa na CHADEMA na kuitelekeza nje ya nyumba yake katika Kijiji cha Nyakunguru.
Aidha, miongoni mwa uhalifu unaodaiwa kutendwa na askari wa kanda hiyo ni tukio la udhalilishaji dhidi ya wanawake wa familia moja katika Kijiji cha Kebweye, Mei  mwaka 2010 tukio lilisosababisha kuundwa tume na  Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema na kusababisha Waziri Mkuu, Mizengo pinda kuomba radhi bungeni.
Akizungumzia suala hilo, Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Matiko, alisema atahakikisha anafungua ofisi ndogo wilayani Tarime na kuweka wakili ili kusaidia kutetea haki za wananchi waliodhulumiwa mikononi mwa jeshi hilo kwa kufuata utaratibu wa kisheria.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa