Mwandishi wetu, Bunda
Moto ulioteketeza mabweni mawili katika shule ya sekondari Ikizu, iliyoko wilayani Bunda, haukusababishwa na hitilafu ya umeme bali inasadikika ni hujuma iliyofanywa na watu wasiofahamika.
Mkuu wa wilaya ya Bunda, Joshua Mirumbe, amewambia waandishi wa habari jana ofisini kwake kuwa kufuatia tukio hilo lililotokea usiku wa kuamkia juzi, ameunda tume ya watu saba kwa ajili ya kuchunguza chanzo cha moto huo.
Mirumbe amesema kuwa inasadikika chanzo cha moto huo, ulioteketeza mabweni mawili yanayotumiwa na wanafunzi 100, ni hujuma iliyofanywa na watu wasiofahamika na hivyo ameamua kuunda tume.
Amesema moto huo haukusababishwa na hitilafu ya umeme kama ilivyoripotiwa awali na kaimu mkuu wa shule hiyo, Emmanuel Masasi, kwa sababu ulianzia sehemu ya chini ambako hakuna umeme.
Amesema kuwa tukio hilo limelotokea usiku wa kuamkia juzi, wakati wanafunzi hao wakiwa madarasani wakisoma na kwamba hakuna mwanafunzi aliyejeruhiwa.
Amesema kuwa tume hiyo, ambayo itashirikisha vyombo vyote vya ulinzi na usalama na wataalamu wa utambuzi wa mambo ya moto, itafanyakazi yake kwa muda wa siku tano, ambapo kazi yake kubwa ni kuchunguza chanzo cha moto huo, kufanya tathmini ya hasara iliyopatikana na kuweka mikakati madhubuti.
Blogzamikoa
Blogzamikoa
0 comments:
Post a Comment