Home » » WAGOMBEA WA CCM MUSOMA MJINI WADAIWA KUANZA RAFU

WAGOMBEA WA CCM MUSOMA MJINI WADAIWA KUANZA RAFU

Na Mwandishi Wetu, Musoma
BAADHI ya wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya Musoma Mjini, wanadaiwa kununuliwa na mmoja wa wagombea wa nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC), kuhakikisha wagombea wengine wanaondolewa ama kupewa alama za chini zitakazofanya wasiteuliwe.

Wakizungumza mjini hapa jana kwa masharti ya kutotajwa majina yao, wagombea hao wamedai kuwa Septemba 3, mwaka huu, baadhi ya wajumbe hao walipewa zaidi ya Sh milioni 10 kupitia kwa kiongozi mmoja wa chama hicho wa Wilaya ya Serengeti, baada ya kuhakikiwa unachama wao.

Walisema baada ya mchakato huo kukamilika, kiongozi huyo aliwachukua wajumbe hao na kuwapeleka katika hoteli moja ya kitalii, kisha kuwapa fedha hizo zinazodaiwa kutolewa na mgombea huyo.

“Kwa kweli tumesikitishwa na kitendo kinachotaka kufanywa na baadhi ya wajumbe wa kamati ya siasa kukiuka taratibu na kanuni za chama, hivi kweli sisi ambao hatuna fedha hatuwezi kuwa viongozi. Iweje mtu mmoja huyo huyo amepanga safu ya uongozi wa kamati ya siasa leo, tena anatoa fedha zote hizo kununua baadhi ya wajumbe ili tusitendewe haki kama wanachama,” walisema wagombea hao.

Hata hivyo, Katibu wa CCM Wilaya ya Musoma Mjini, Musa Matoroka, alisema si kweli kwamba kuna mgombea amenunua baadhi ya wajumbe, ila chama kimekuwa kikiomba michango kwa hiari kwa wagombea, wanachama na watu wengine wenye mapenzi na chama chao.

“Hakuna kitu kama hicho cha wajumbe kununuliwa, ofisi yetu ina utaratibu maalumu na hata ukifika ofisini kwangu utakuta kuna kadi za michango, tunaomba kwa mtu binafsi, wanachama, wakiwamo wagombea na kampuni tena hiari hakuna anayelazimishwa kuchanga,” alisema Matoroka.

Pamoja na kukanusha madai hayo, baadhi ya wajumbe wa kamati ya siasa ya Musoma Vijijini wamethibitisha wajumbe wenzao kuhongwa fedha hizo katika kuhakikisha wagombea wengine wanaenguliwa mapema ama kupewa alama za chini zaidi.

“Kweli fedha hizo zimetolewa kwa baadhi ya wenzetu na sisi wengine tumebaguliwa kwa kuwa walikuwa wanaangalia msimamo wa kila mjumbe, anaweza kuunga mkono wazo lao kwa kuzingatia idadi kubwa ya wajumbe watakaowaunga mkono,” alisema mjumbe mmoja na kuongeza:

“Kama kweli chama hiki kinaendeshwa na mtu mmoja kwa fedha zake tulichokipata mwaka 2010 hadi kupoteza jimbo, tujiandae kukipata mwaka 2015 kwa kuwa huwezi kuwaondoa wagombea eti kwa vile tu ni masikini na hawana fedha za kuhonga watu,” alisema.

Baadhi ya wagombea wa nafasi hiyo ni Dora Jama, Emanuel Bwimbo, Mdari Kerenge, Athuma Kitwara, Magoti Kamese na Vedastus Mathayo, anayetetea nafasi hiyo baada ya kuwa mjumbe wa NEC Mkoa wa Mara kwa miaka mitano.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa