FAMILIA ya watu 19 wilayani Bunda, mkoani Mara, hawana
mahali pa kuishi baada nyumba zao tano kubomolewa kutokana na amri ya mahakama
ya baraza la nyumba na ardhi katika wilaya ya Musoma, kwa kile kilichodaiwa
kuwa mmiliki wa nyumba hizo alikuwa amevamia ardhi ya mtu mwingine.
Tukio hilo limetokea juzi katika kijiji cha Guta B, wilayani
humo, ambapo nyumba hizo ni mali ya Hitinde Chacha, mkazi wa kijiji hicho
ambaye ana familia ya watu 19.
Mwenyekiti wa kijiji cha Guta B, Bw. Kisheri Miyange,
amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kwamba kwa sasa wanafamilia hao wakiwemo
watoto wadogo wanalala nje.
Bw. Miyange amesema kuwa siku ya tukio dalali mmoja akiwa na
askari polisi walifika kijijini hapo na kusema kuwa wanazibomoa nyumba hizo kwa
idhini ya baraza la nyumba na ardhi, kwa sababu mmiliki wa nyumba hizo alivamia
ardhi ya mwananchi mwingine.
Amesema kuwa walikodi vijana waliowasaidia kubomoa nyumba
hizo pamoja na maghara ya kuhifadhia vyakula.
Mmiliki wa nyumba hizo, Bw. Hitinde Chacha amesema kuwa
wakati nyumba zake zinabomolewa yeye pamoja na wake zake hawakuwepo bali
kulikuwa na watoto wadogo.
Bw. Chacha amesema kuwa baadhi ya vitu vyake vimeporwa na
wabomoaji hao zikiwemo fedha tasilimu alizokuwa ameuza ng’ombe wake na kwamba
chakula kilichokuwa magharani kimeharibiwa na watu hao.
Aidha, amesema anawasiliana na watu wa haki za binadamu
kutoa kilio chake kwani hakutendewa haki.
Mwenyekiti wa baraza la nyumba na ardhi wilayani Musoma hakupatikana
kuzungumzia suala hilo, na juhudi za kumtafuta bado zinaendelea.
0 comments:
Post a Comment