MWANAUME mmoja ameuawa na
wananchi wenye hasira wilayani Tarime katika mkoa wa Mara, kwa tuhuma ya kuiba
ng’ombe mmoja mwenye thamani ya shilingi laki tatu.
Kamanda wa polisi katika kanda
maalumu ya Tarime na Rorya, kamishina msaidizi wa polisi, Bw. Justus Kamugisha,
amemtaja mwanaume huyo kuwa ni John Mang’era Hirengo (38) mkazi wa kijiji cha
Kwisarara wilayani Tarime.
Kamanda Kamugisha amesema kuwa
tukio hilo limetokea juzi majira ya saa 6:00 usiku, katika kijiji cha Kwisarara
wilayani humo na kwamba alituhumiwa kuiba ng’ombe mmoja mali ya Wakuru Chacha
Mayombo mkazi wa kijiji hicho.
Amesema kuwa baada ya kuiba
ng’ombe huyo wananchi wenye hasira walimfuatilia na kufanikiwa kumkamata akiwa
na ng’ombe huyo na ndipo wakamshushia kipigo kikali kilichoondoa uhai wake.
Ameongeza kuwa marehemu mara
kwa mara alikuwa akituhumiwa kuwa ni mwizi sugu wa mifugo katika eneo hilo.
Aidha, amesema kuwa kufuatia
tukio hilo hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa kuhusiana na mauwaji hayo na polisi
bado wanaendelea na upelelezi juu ya tukio hilo.
0 comments:
Post a Comment