Home » » Polisi Tarime wagundua mashamba ya bangi, wayafyeka na kuchoma moto

Polisi Tarime wagundua mashamba ya bangi, wayafyeka na kuchoma moto

JESHI la polisi katika kanda maalumu ya Tarime na Rorya wamefanikiwa kugundua mashamba mawili ya bangi na kuyafyeka na kisha mmea huo kuuteketeza kwa moto.

Kamanda wa polisi katika mkoa wa kipolisi wa Tarime na Rorya, Bw. Justus Kamugisha, amesema kuwa tukio hilo limetokea juzi katika kitongoji cha Bumera kijiji cha Kwisarara wilayani Tarime.

Amesema kuwa polisi wakiwa katika msako wa kusaka wahalifu waligundua mashamba mawili ya bangi yenye ukubwa wa ekari tatu na nusu na kwamba kama bangi hiyo ingevunwa ingekuwa na uzito wa kilo 8,200.

Amesema kuwa mashamba hayo ni mali ya mwanamke mmoja Bhoke Mwita na mwanaume mmoja Mang’era Wambura, ambao wote ni wakazi wa wilayani Tarime, na kwamba wote wametoroka na wanatafutwa na polisi.

Aidha amesema kuwa baada ya kugundua mashamba hayo, polisi waliyafyeka na kuiteketeza kwa moto bangi hiyo na kwamba sasa wanawasaka watuhumiwa ili wawafikishe kwenye sheria.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa