na Berensi Alikadi, Musoma
MBUNGE wa Musoma Mjini, Vincent
Nyerere (CHADEMA), amewataka vijana katika jimbo hilo kujiunga na kuanzisha
vikundi mbalimbali ili iwe rahisi kupewa mikopo itakayowasaidia kujiendeleza
kiuchumi.
Nyerere alitoa ushauri huo jana
alipozungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho Kata ya Kitaji katika
mkutano uliofanyika Shule ya Msingi Musoma.
Alisema njia pekee ya vijana
kujikwamua katika umaskini ni kuanzisha vikundi na kuvisajili, ili waweze
kuomba mikopo kutoka serikalini na kwenye taasisi za kifedha.
Alisema yeye kama mbunge hayuko
tayari kugawa pesa kwa kila kijana, kwani si sera ya chama chake, bali
atakachofanya ni kuwasaidia vijana namna ya kuandika michanganuo mbalimbali kwa
ajili ya kupata mikopo.
“Nataka niwaambie vijana wenzangu,
mimi sitaweza kugawa sh 50,000 kwa kila kijana wa jimbo hili, uwezo huo sina,
lakini pia si sera ya CHADEMA, bali nawaomba vijana mjiunge katika vikundi na
mvisajili ili niweze kuwasaidia namna ya kupata pesa kutoka kwa wafadhili,’’
alisema Nyerere.
Katika hatua nyingine, mbunge huyo aliwataka
wanachama wa chama hicho kuachana na maneno ya propaganda zinazoenezwa na Chama
Cha Mapinduzi (CCM) kuwa hajafanya kitu na kwamba wananchi wanaona tofauti
iliyopo kati yake na mbunge aliyetangulia.
CHANZO TANZANIA DAIMA
0 comments:
Post a Comment