Home » » Wananchi Bunda waingiliwa usiku na watu wasiojulikana, milango yafunguliwa bila kujua, wafanyiwa vitendo vichafu

Wananchi Bunda waingiliwa usiku na watu wasiojulikana, milango yafunguliwa bila kujua, wafanyiwa vitendo vichafu

WANANCHI wa kijiji cha Kasahunga wilayani Bunda, mkoani Mara, sasa wanaishi maisha ya wasiwasi, kutokana na kuibuka kwa kikundi cha watu wasiofahamika, ambao uwaingilia kwenye nyumba zao nyakati za usiku bila kujua na kufanya uporaji wa vitu mbalimbali na kutaka kubaka wanawake.

Matukio ya watu kuingiliwa kwenye nyumba zao bila kujua yametokea usiku wa kuamkia jana katika kijiji cha Kasahunga, ambapo kikundi cha watu hao kimeingilia kaya zaidi ya 20 na kufanya uporaji wa simu za mikononi na pesa tasilimu na kutaka kubaka wanawake.

Watu ambao wameingiliwa na kikundi hicho wamesema kuwa licha ya kuwa wamefunga milango ya nyumba zao vizuri, walishitukia mtu mmoja ambaye alikuwa amenyoa upara, akiwa amevaa bukuta bila shati, akiwa amewaingilia ndani ya vyumba vyao na kutaka kubaka wananwake.

Aidha, wananchi hao wamesema kuwa katika miji mingine kikundi hicho kilifungia kwa nje milango ya nyumba za majirani ili wasitoe msaada na kuingia kwenye nyumba za wananchi hao na kufanya uporaji wa pesa tasilimu na simu za mkononi na kisha kutokomea kusiko julikana.

Kufuatia hali hiyo wananchi wa kijiji cha Kasahunga, sasa wanaishi kwa wasiwasi huku wakiyahusisha matukio hayo na mambo ya ushirikina, lakini baadhi wakidai kuwa pamoja na ushirikina hicho ni kikundi cha vibaka tu.

Mkuu wa wilaya ya Bunda, Bw. Joshua Mirumbe, amekemea hali hiyo kwa ni uvunjifu wa amani na ameagiza afisa tarafa ya Kenkombyo na kamati ya ulinzi na usalama ya kata ya Neruma, pamoja na uongozi wa kijiji cha Kasahunga kuchukua hatua za haraka kudhibiti hali hiyo mara moja.

Kijiji cha Kasahunga kimekuwa na matukio ya ajabu yanayohusishwa na imani za ushirikina, kwani hivi karibuni wanawake watatu waliuawa na nyumba zao kuchomwa moto, wakituhumiwa kuwa ni wachawi.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa