WILAYA ya Bunda, mkoani Mara kupitia shirika lisilo
la kiserikali lijulikalo kama MAF, limefunga mashine tatu za kukamulia alizeti
katika kata tatu za wilaya hiyo, ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kupambana
na umaskini.
Kata zilizofungwa mashine hizo ni Mugeta na Bunda,
zilizoko Tarafa ya Serengeti na Kata ya Kibara iliyopo Tarafa ya Nansimo.
Akizungumza katika uzinduzi wa mashine hizo
mwishoni mwa wiki katika Kijiji cha Mugeta, Mwenyekiti Mtendaji wa shirika
hilo, Respice Mkama, alisema lengo la mradi wao ni kuwawezesha wakulima wa zao hilo
kukamua na kuuza mafuta yao.
Alieleza kuwa mashine hizo aina ya Whriston kutoka
China zimegharimu zaidi ya sh milioni 40, zina uwezo wa kukamua tani tano hadi
nane kwa siku na kwamba ana imani wakulima wa kata hizo watanufaika na
kuondokana na umaskini.
“Katika utafiti wetu tuliofanya tuliona alizeti
inasitawi katika maeneo ya kata hizo na ni zao zuri linaloweza kuwaondolea
umaskini badala ya kulima pamba pekee,” alisema.
Mkama alisema zao hilo linaweza kukomaa kwa miezi
mitatu na kila gunia lina uwezo wa kutoa lita 25 za mafuta, hivyo kuwataka
wakulima wa maeneo hayo kuchangamkia fursa hiyo, kwani kuna soko la uhakika.
Ofisa Kilimo wa halmashauri hiyo, Balisimaki Shija,
alisema kupitia agizo la mkuu wa wilaya hiyo alilotoa wiki iliyopita ni lazima
kila mkulima alime ekari mbili za zao hilo kama zao la biashara licha ya kuwapo
zao la pamba.
Alisema halmashauri hiyo itatoa mbegu za ruzuku kwa
wakulima, hivyo akawatoa wasiwasi wakulima na kuwataka walime zao hilo kwa
wingi.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Joseph Malimbe,
ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo alisema alizeti ni zao
linaloongeza tija kwa wakulima katika mazao ya biashara.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment