KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),
Abdulrahman Kinana, amempa muda wa wiki mbili Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime
mkoani Mara, John Henjewele, kuonana na kampuni ya uchimbaji madini ya dhahabu
ya Barrick North Mara kupata majibu ya madai kwamba imeacha kutoa asilimia moja
ya mapato yatokanayo na uzalishaji wa dhahabu.
Malipo hayo ni kwa ajili ya ada kwa wanafunzi wa
vyuo vikuu, na kuna taarifa kwamba mkataba wa fedha hiyo ulikwisha, wakati
uliopo unaitaka kampuni hiyo kutoa kila mwaka hadi mwisho wa uhai wa mgodi huo.
Kinana alifikia hatua hiyo, baada ya kusomewa
risala iliyoandaliwa na viongozi wa CCM kata za vijiji saba vilivyoingia
mkataba huo.
Katika mkutano huo uliofanyika katika viwanja vya
stendi vya Nyangoto, Kinana alisema ametoa muda huo ili mkuu huyo wa wilaya
ahakikishe anapatiwa majibu sahihi na kampuni hiyo.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Nishati na
Madini, Stephen Masele ameitaka Barrick kuhakikisha wanajenga barabara ya
kiwango cha lami kutoka Tarime hadi mpakani mwa wilaya hiyo na Serengeti katika
kijiji cha Murito, kutekeleza makubaliano yaliyowekwa na vijiji vya mgodi huo.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment