RAIA wa China, Chen Weitao, dereva wa Kampuni ya
ujenzi ya Chico inayotengeneza barabara ya Musoma-Mwanza, amekamatwa na askari
wa Kikosi cha Kudhibiti Ujangili akiwa na mfupa uliokauka wa mguu wa tembo.
Weitao alikamatwa juzi, majira ya saa sita mchana,
eneo la Nyasura katika mji mdogo wa Bunda.
Ofisa mmoja wa kikosi hicho Kanda ya Serengeti
ambaye hakutaka kutajwa jina alisema walipata taarifa kutoka kwa raia mwema.
Alisema baada ya kupata taarifa hiyo walikwenda
moja kwa moja eneo hilo na kumkuta Weitao akiwa na gari T 340 BBR na baada ya
kulikagua walikuta mfupa huo ukiwa kwenye sehemu ya kutunzia spana.
Alisema walimkamata raia huyo wa China aliyekuwa na
msaidizi wake aitwaye, Michael Renatus, na kuwapeleka kituo cha polisi ambako
waliwaweka chini ya ulinzi na kuwahoji.
Raia huyo wa China alidhaminiwa juzi baada ya
kukabidhi hati yake ya kusafiria katika Kituo cha Polisi Bunda na kupewa gari
lake ingawa ataendelea kuhojiwa na kikosi hicho.
Hii ni mara ya nne sasa kwa Wachina hao kukamatwa
na nyara za serikali tangu waanze kujenga barabara hiyo, ambapo mwaka jana
walikamatwa na vipande vya meno ya tembo katika kambi yao iliyopo Sabasaba.
Polisi wilayani hapa wamekiri kukamatwa kwa Mchina
huyo na kudai suala hilo linasimamiwa na Kikosi cha Kuzuia Ujangili Kanda ya
Serengeti, ambao kwa hivi sasa wana wanasheria wao ambao wanaandaa mashitaka na
kuwafikisha mahakamani watuhumiwa hao.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment