Home » » Madiwani Bunda waonywa kutokujihusiha na biashara katika halmashauri hiyo

Madiwani Bunda waonywa kutokujihusiha na biashara katika halmashauri hiyo

KUTOKANA na baadhi ya madiwani kujihusisha na biashara katika halmashauri zao, mkuu wa mkoa wa Mara Bw. John Tupa, amewaonya madiwani wote mkoani humo, kuacha mara moja tabia hiyo kwani ni kunyume na utaratibu wa uongozi.

Mkuu huyo wa mkoa wa Mara ameyasema hayo jana kwenye kikao maalum cha baraza la madiwani cha kujadili hoja za mkaguzi na mdhibiti mkuu wa fedha za serikali, kilichofanyika mjini Bunda.

Katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na mkuu wa wilaya ya Butiama, Bi. Angelina Mabula, mkuu huyo wa mkoa amesema kuwa baadhi ya madiwani wamekuwa wakifanya biashara na halmashauri zao kwa kuchukua tenda za miradi mbalimbali ya maendeleo.

Mkuu wa mkoa amesema kuwa hali hiyo imekuwa ikisababisha miradi husika kutokuwa na kiwango kinachotakiwa ikilinganishwa na fedha zilizotengwa, sanjari na miradi kutokamilika kwa wakati uliopangwa.

Hata hivyo mkuu wa mkoa wa Mara ameipongeza halmashauri hiyo kupata hati inayoridhisha, lakini hakaonya kuwa sio vizuri kuwa na hoja za ukaguzi zinazojirudia mara kwa mara katika halmashauri hiyo.

Katika kikao hicho madiwani wameshangazwa na ujenzi wa ofisi za kata kutokukamilika kwa wakati, ikiwa ni pamoja na soko la mji mdogo wa Kibara kutokukamilika, ambapo fedha sh. milioni 10 zinadaiwa zimetafunwa katika mazingira ya kutatanisha.

Hata hivyo mratibu wa mradi wa TASAF wilayani Bunda, Bw. Mshingi Baragi amekanusha tuhuma hizo na kusema kuwa fedha zote za mradi wa soko hilo zilipelekwa na kufanya kazi iliyokusudiwa na kwamba kazi ya mradi huo imekamilika kama ilivyokuwa imepangwa na kuongeza kuwa kinachotakiwa sasa ni wananchi kujenga vibanda kwa ajili ya kuzunguka soko hilo.

Akihahirisha kikao hicho mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Bunda, Bw. Joseph Marimbe, amesema kuwa watahakikisha kasoro zote zinaondolewa kadiri ya uwezo wao kwa sababu hakuna sababu ya hoja za ukaguzi kujirudiarudia mara kwa mara.

Bw. Marime amesema kuwa pale ambapo itawezekana kufanya vibaya watachukuliana hatua kwa wale wanaohusika, kwa sababu hakuna haja ya hoja hizo kujirudiarudia mara kwa mara.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa