Home » » ‘Mungiki’ wavamia Mkoa wa Mara, Usalama wa raia, mali zao mjini Musoma shakani, Wananchi wamwita RPC ‘Kamanda wa Biashara’

‘Mungiki’ wavamia Mkoa wa Mara, Usalama wa raia, mali zao mjini Musoma shakani, Wananchi wamwita RPC ‘Kamanda wa Biashara’

WAKAZI wa Mkoa wa Mara hususan Musoma Mjini wanaishi katika hali ya hofu kubwa kutokana na wingi wa vitendo vya uporaji, uvamizi na ubakaji vinavyoendeshwa na vikundi vitatu vya vijana.

Vikundi hivyo vyenye uhasama miongoni mwao, vinajulikana na wakazi wa Musoma na katika hali ya kushangaza vimekuwa vikiendesha matukio ya kihalifu bila kuingiliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo.

RAI limebaini kuwa vikundi hivyo maarufu kama Midomo ya Furu, Jamaica na Mbio za Vijiti vinaundwa na vijana wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 25, na huvamia maduka kisha hufanya unyang’anyi kwa kutumia silaha na hata kuua.

“Ukikutana nao usiku unaweza kudhani labda ni kundi la vijana walemavu kwani hutembea bila kukunja magoti ya miguu yao ya kulia kutokana na visu virefu na nondo wanazokuwa wamechomeka kwenye suruali kuanzia kiunoni.

“Ni hofu tupu. Ikifika saa moja jioni huwezi kutembea mitaani. Vijana hawa wana nguvu kubwa na ni wazi kuwa polisi wameshindwa kabisa kuwadhibiti na sasa hakuna mwenye imani na jeshi hilo,” mkazi mmoja wa eneo la Nyakato CCM mjini Musoma aliliambia gazeti hili.

Alisema kutokana na kukosa imani kwa polisi, Kamanda wa Polisi Mara, Ferdinand Mtui, amepachikwa jina la ‘Kamanda wa Biashara’ na wakazi wa Musoma.

“Ni kwa sababu Kamanda Mtui na vijana wake wamekuwa wakikimbizana na wafanyabiashara mchana kutwa na kuwatoza fedha, lakini usiku ukiingia, hawaonekani mitaani, wanawaacha Midomo ya Furu na wenzao wakitamba,” alisema.

Makundi hayo yamekuwa yakifanya uhalifu kuanzia saa moja jioni hadi saa 11 alfajiri, wakiivamia nyumba waliyokusudia, huziweka nyumba nyingine zote jirani chini ya ulinzi hadi watakapomaliza kazi ili kuwazuia kutoa msaada.

Wakati mwingine vijana hao hupanda kwenye mapaa ya nyumba au maduka waliyoyalenga na kutoboa bati, kisha huingia ndani na kufanya uhalifu.

RAI lilishuhudia nyumba nyingi za wakazi wa Musoma hasa wa maeneo ya Nyakato CCM, Nyakato Madukani, Nyakato Kanisani, Magamaga, Maduka Saba na Kwa Saa Nane zikiwa ama zimetobolewa mabati, kuta za matofali au uharibifu wa aina nyingine.

Oktoba 15 mwaka huu eneo la Nyakato, RAI lilimshuhudia Gabu, kijana wa kundi la Mbio za Vijiti, akichomwa kisu na kufa na vijana wa kundi jingine hasimu.

Siku ya mazishi yake, wanakikundi wenzake walizua tafrani kwa kuuteka mwili na wakati wakitokomea nao kusikojulikana, polisi waliingilia kati na kuwatawanya kwa mabomu ya machozi hivyo kulitelekeza jeneza lililokuwa na mwili wa kijana huyo. 

RPC ageuka bubu:

Juhudi za kumpata RPC Mtui kuzungumzia kadhia hiyo zilishindikana kwa siku nne mfululizo, kwani hakupokea simu hata baada ya mwandishi kujitambulisha kupitia ujumbe mfupi wa maandishi.

RAI lililazimika kuripoti kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema, ambaye simu yake ilipokewa na msaidizi wake aliyeshauri tuwasiliane na Msemaji wa jeshi hilo, Advera Senso ambaye naye hakupokea simu.

Baadaye, RAI lilifanikiwa kuzungumza na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Robert Manumba, aliyesikitishwa na uduni wa usalama huko Musoma.

Katika kile kinachoonekana kama kushinikizwa na mabosi wake kutoka Dar es Salaam kuzungumza na RAI, RPC Mtui aliibuka ghafla na kupiga simu chumba cha habari Dar es Salaam akitaka kuonana na mwandishi wetu, Shomari Binda wa Musoma.

“Mimi huwa sizungumzi kwa simu na mtu nisiyemfahamu, mwambie mwandishi wenu wa Musoma aje ofisini. Kama huwa mnazungumza na makamanda wengine kwa simu, hiyo ni formula yao, sio mimi,” alisema baada ya kuambiwa kwamba RAI huzungumza na maofisa mbalimbali hata kwa simu bila matatizo, iweje yeye hataki.

Baadaye, alimwambia mwandishi huyo kwamba polisi mkoani Mara kwa kushirikiana na wananchi limefanikiwa kuvidhibiti vikundi hivyo, na wengi kati yao wako magereza wakikabiliwa na makosa mbalimbali.

Alikiri kuwapo kwa makundi hayo ya kihalifu akisema ilikuwa ni siku za nyuma lakini vimesambaratishwa.

“Changamoto iliyopo ni kuwapo mtaani kwa wanafunzi zaidi ya 45,000 waliomaliza elimu ya msingi ambao baadhi yao wamekuwa na mambo ya kuiga.

“Suala la kuwapo vikundi vya kihalifu si la Jeshi la Polisi pekee, kwani vijana wengi wapo mitaani, hawana kazi hivyo maswali mengine wanaweza kuulizwa viongozi wengine kwa nafasi zao katika jamii,” alisema.

Alisema jeshi hilo limeanzisha kikosi maalumu kupambana na uhalifu kwa ushirikiano wa karibu na wananchi, hivyo kupunguza matukio hayo kwa kiwango kikubwa na kuwaondolea hofu wananchi.

Hata hivyo, habari zilizolifikia gazeti hili jana kutoka Musoma zilisema maiti mbili zimekutwa katika eneo la Kwangwa, Musoma Mjini baada ya kuchinjwa watu wasiofahamika.

Moja kati ya maiti hizo ilikutwa ikiwa imeanza kuharibika. Watu wanayemfahamu waliliambia RAI kwamba aliaga nyumbani kwake kuwa anakwenda Bisumwa wiki moja iliyopita na hakuonekana tena.
Chanzo: Rai

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa