Home » » LHRC yalia na operesheni ya majangili

LHRC yalia na operesheni ya majangili

Mkurugenzi wa Maboresho na Utetezi wa LHRC,Harold Sungusia
Kituo  cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimeitaka serikali kufunga kambi maalumu za kutesa watuhumiwa wa makosa ya ujangili zilizoanzishwa katika mbuga ya Serengeti mkoani Mara kwa kuwa hatua hiyo ni ukiukwaji wa haki za binadamu na uvunjaji wa Katiba ya nchi.
Moja ya kambi hizo imepewa jina la Guantanamo iliyopo eneo la Handageja na nyingine inaitwa Lemai ambayo inadaiwa mtu aliyefahamika kwa jina la Rwegesa Iselega, mkazi wa Lemanga aliteswa na kufariki dunia.

Mkurugenzi wa Maboresho na Utetezi wa LHRC, Harold Sungusia alitoa kauli hiyo kupitia tamko la kituo hicho alilolisoma kwa niaba ya Mkurugenzi mtendaji, Dk. Hellen Kijo-Bisimba.

Sungusia alisema kuna ukiukwaji mkubwa katika Operesheni ya Tokemeza ujangili na kwamba Ofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), alihusika kusaini hati ya kiapo kwa ajili ya kuwapeleka mahakamani watuhumiwa 13, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Kituo hicho kimesema kambi hizo za kutesa wananchi zinasimamiwa na maofisa wa JWTZ na kwamba wananchi wamekuwa wakipigwa, kumwagiwa pilipili pamoja na kutishiwa bunduki ili wakiri makosa yao.
Sungusia alisema zoezi hilo limekiuka misingi ya utawala wa sheria na haki za binadamu kwani ibara ya Katiba ya nchi ya mwaka 1977 ibara ya 13(6)(e) inaeleza kwamba ni marufuku mtu kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazomtweza au kumdhalilisha.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa