Home » » JELA MIAKA 30 KWA UNYANG`ANYI WA KUTUMIA SILAHA

JELA MIAKA 30 KWA UNYANG`ANYI WA KUTUMIA SILAHA

MAHAKAMA ya wilaya ya Serengeti Mkoani Mara imemhukumu Nyaitore Mbota(20) mkazi wa Rebu wilaya ya Tarime kwenda jela miaka 30 baada ya kumtia hatiani kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha. Hakimu wa mahakama hiyo Franco Kiswaga akitoa hukumu amesema ushahidi uliotolewa mahakamani hapo umemtia mtuhumiwa huyo hatiani na kuwa anastahili kutumikia adhabu hiyo ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hizo. Mapema mwendesha mashita wa polisi mkaguzi msaidizi wa polisi Alfred Marimi, ameiambia mahakama kuwa mshitakiwa ametenda kosa hilo machi 4 mwaka 2010 majira ya saa 1 usiku eneo la mnada wa zamani mjini mugumu baada ya kukodisha pikipiki aina ya Toyo yenye namba za usajili T245BDN, yenye thamani ya shilingi 1,400,000/= mali ya Magutu Kitera. Na kuwa mshitakiwa baada ya kufika eneo hilo alimuomba bodaboda huyo asimamishe pikipiki ili amlipe nauli, baada ya kusimama alimpiga nyundo kichwani na kuanguka na kuchukua pikipiki, hata hivyo wananchi walizingira na kumkamata na kumfikisha kituo cha polisi Mugumu. Mwendesha mashitaka ameiomba mahakama itoe adhabu kali kwa mshitakiwa ili iwe fundisho kwa wengine kutokana na kukithiri kwa vitendo vya unyang`anyi wa pikipiki.. Katika utetezi wake Mbota ameomba mahakama imuonee huruma kwa kumpunguzia adhabu kwa kuwa amesingiziwa na anategemewa na wazazi wake, hata hivyo hakimu ametupilia mbali utetezi huo na kumpa adhabu hiyo na rufaa iko wazi kama hajaridhika.



0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa