Home » » Wanachuo wakabiliwa na ugonjwa wa homa ya matumbo kwa kunywa maji machafu

Wanachuo wakabiliwa na ugonjwa wa homa ya matumbo kwa kunywa maji machafu


WANANCHUO cha maendeleo ya wananchi Kisangwa kilichoko wilayani Bunda, mkoani Mara, wanakabiliwa na magonjwa mbalimbali, ukiwemo wa homa ya matumbo kutokana na kutumia maji yasiyokuwa salama kwa afya za binadamu.
 
Mkuu wa chuo cha maendeleo ya wananchi Kisangwa, Bw. Emilian Mrosso, ameyasema hayo jana kwenye mahafali ya 17 ya kuhitimu fani ya ufundi, uashi, kilimo na mifugo, ambapo wahitimu 37 kati ya 73 walioanza masomo hayo wamekabidhiwa vyeti vyao.
 
Bw. Mrosso amesema kuwa wanachuo hao wanakabiliwa na changamoto hiyo, kwani maji wanayotumia ni ya kwenye lambo, ambalo linatumiwa na mifugo, ambalo liko umbari wa kilomita tatu.
 
Amesema kuwa kutokana na tatizo hilo wanachuo wengi wamekuwa wakiugua magonjwa mbalimbali, ukiwemo wa homa ya matumbo na kichocho, na kwamba kutokana na kunywa, kuoga na kutumia maji hayo katika matumizi ya binadamu hali hiyo husababisha baadhi ya wanachuo kukatisha masomo yao.
 
Mganga mkuu wa chuo hicho, Dk. Ally Odiambo, amesema kuwa kwa kipindi cha miezi miwili, wanachuo watano wamekuwa wakiugua ugonjwa huo kwa kutumia maji yasiyokuwa salama.
 
Mgeni rasmi katika mahafali hiyo, aliyemwakilisha mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Bunda, Bw. Charles Machage, amesema kuwa amezichukua changamoto hizo, ikiwemo ya kutokuwepo barabara ya kufika chuoni hapo na kwamba zitafanyiwa kazi mara moja.
 
Wanachuo 73 walianza masomo chuoni hapo, lakini ambao wamehitimu ni 35 tu, kutokana na wengine kukatisha masomo yao kwa changamoto hio ya maji.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa