KIKUNDI cha Wapiga Makasia cha Nyarusurya Wanaume kutoka Musoma
Mjini mkoani Mara, kimetwaa ubingwa wa mashindano ya mbio za Mitumbwi
zinazodhaminiwa na Balimi Extra Lager hivyo kujitwalia zawadi ya fedha
taslimu sh 900,000 na tiketi ya kuwakilisha mkoa katika Ngazi ya Kanda
inayotarajiwa kufanyika jijini Mwanza hivi karibuni.
Nafasi ya pili, ilichukuliwa na kikundi cha nahodha Bernard kutoka
Kinesi ambao walizawadiwa sh 700,000 huku nafasi ya tatu ikichukuliwa
na kikundi cha nahodha Benedkito Chamba kutoka Bwai waliozawadiwa sh
500,000 wakati kikundi cha Mweme kutoka Kinesi, walishika nafasi ya nne
na kujitwalia sh 400,000. Nafasi ya sita hadi kumi walipewa kifuta
jasho cha sh 250,000 kwa kila kikundi.
Upande wa wanawake, Kisorya Group kutoka Kisorya Bunda ambao walikuwa
mabingwa wa kanda mwaka jana, kilitwaa ubingwa na hivyo kuzawadaiwa sh
700,000 pamoja na tiketi ya kuwakilisha mkoa wa Mara kwenye mashindano
ya kanda pale jijini Mwanza mwezi ujao.
Nafasi ya pili ilichukuliwa na kikundi cha Nyamiti kutoka Majita,
ambao walijinyakulia sh 600,000 pamoja na kuwakilisha kwenye fainali za
kanda huku nafasi ya tatu ikienda kikundi cha Mama Lameck kutoka
Lukuba ambao walizawadiwa sh 400,000 wakati nafasi ya nne ikichukuliwa
na kikundi cha Rhobi kutoka Kinesi walioondoka na sh 300,000.
Akizungumza, mgeni rasmi katika mashindano hayo, Mkuu wa Upelelezi
Wilaya ya Musoma, Juma Mataka, wakati wa kukabidhi zawadi mbalimbali
kwa washindi wa shindano hilo, alisema kuwa Kampuni ya Bia Tanzania
(TBL), kwa kutambua umuhimu wa mashindano hayo kupitia bia yake ya
Balimi, wameamua kuyaboresha ili kuwawezesha washiriki kujiingizia
kipato.
Naye Mwakilishi wa TBL, Meneja Mauzo wa Kanda ya Ziwa, Malaki Sitaki,
alisema kuwa Kampuni ya Bia Tanzania imeamua kutengeneza ajira kupitia
mashindano ya kupiga kasia ili kuwawezesha wavuvi kujiingizia kipato
na kuweza kuheshimika kwani ajira hiyo imetupwa na watu wengi kutokana
na wahusika kuonekana katika jamii kuwa ni watu walioshindwa maisha.
Fainali za kanda za mashindano hayo zinatarajiwa kufanyika Desemba 7
mwaka huu ufukwe wa Mwaloni jijini Mwanza, ambako watashindana mabingwa
kutoka Kigoma, Kagera, Ukerewe, Musoma na wenyeji Mwanza.
Chanzo; Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment