Bunda. Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, mkoani
Mara, inakusudia kuwashtaki mahakamani, Wachina wanaokarabati kwa
kiwango cha lami, Barabara ya Musoma - Simiyu kutokana na kitendo chao
cha kuchimba madini ndani ya eneo la halmashauri hiyo bila kulipa fidia.
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Simon
Mayeye, alisema Wachinahao kupitia kampuni yao ya ujenzi, walivamia
Vitongoji vya Balili Chini na Bigutu vya wilayani humo na kuanza
kuchimba madini bila idhini ya mamlaka husika.
Alisema “kwa mujibu wa sheria, kila mkandarasi
anayetaka kuchimba madini anapobaini mahala yalipo, lazima awasilishe
mikakati aliyo nayo kuhusu kuwalipa fidia waathirika na kwamba hatua
hiyo inapaswa kufanyika kabla hajaanza kuyachimba.”
Mkurugenzi huyo alisema hata hivyo Wachina hao hawakufanya hivyo.
Mayeye alisema tayari halmashauri yake
imeshawaandikia Wachina hao kuwataarifu juu ya nia ya kuwafikisha
mahakamani kwa kosa hilo.
Mwanasheria wa halmashauri hiyo, Phillip Shoni
alisema suala la ulipaji wa fidia kwa madini ya ujenzi ambayo ni chokaa,
mawe na mchanga, limeainishwa katika sheria namba 14 ya madini
inayotakiwa kuheshimiwa na wadau wote wa ujenzi .
Shoni alisema hata hivyo Wachina hao kwa upande wao, wameshindwa kutekeleza matakwa ya sheria hiyo.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment