Home » » Muhongo awashukia watendaji wabovu

Muhongo awashukia watendaji wabovu

Serengeti. Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema kuwa watumishi wa Serikali ngazi za juu ni chanzo cha kusababisha wananchi kuichukia Serikali iliyopo madarakani na chama chake, kutokana na utendaji kazi mbovu.
Kauli hiyo ilitolewa na waziri huyo jana kwenye kikao cha majumuisho ya ziara yake ya siku tatu mkoani Mara katika Wilaya za Butiama, Bunda na Serengeti kwa madhumuni ya kutembelea mradi wa umeme unaosambazwa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA).
Waziri alifikia hatua ya kutoa kauli hiyo baada ya kupata malalamiko kutoka kwa wananchi vijijini kuwa Serikali inawanyang’anya ardhi na kuwapatia matajiri kwa madhumuni ya kuchimba madini, huku wao wakibaki bila ardhi wala kupewa fidia.
Muhongo baada ya kupata malalamiko hayo alimtaka ofisa madini mkoa kwa kushirikiana na ofisa madini kanda pamoja na viongozi wa halmashauri kuhakikisha wananchi hao wanarejeshewa ardhi yao mara moja.
“Januari 15 mwaka 2014, nyie viongozi wahusika mwitane na mkutane katika vijiji vyote vilivyo na matatizo ya aina hii, mhakikishe mnatatua tatizo, msiwanyanyase wananchi kwa kuwa ni maskini, mnawanyang’anya ardhi yao sasa wao waende wapi?
Wananchi hao walisema wamekuwa wakipokonywa ardhi yao bila wao kuwa na taarifa na kwamba kila wanapohoji hupewa majibu ya kukatisha tamaa.
Mama aliyejitambulisha kwa jina la Mam Suzi mkazi katika kijiji cha Maji moto Wilaya ya Serengeti alidai kuwa yeye ni mjane, ambaye alinyang’anywa ardhi yake na maofisa madini ambapo ardhi hiyo ilikabidhiwa mikononi mwa Kampuni ya Kuchimba Madini ya Bismack.
“Nilinyang’anywa ardhi hivihivi, kwa sababu walikuja watu wakaanza kupima eneo langu, nilipowauliza waliniambia wametumwa na Serikali.
Chanzo;Mananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa