Home » » Mbunge Lugola amshambulia Profesa Msolla

Mbunge Lugola amshambulia Profesa Msolla

Mbunge wa Mwibara,Kangi Lugola
 
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM) amemshambulia Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, ambaye ni Mbunge wa Kilolo (CCM), Profesa Peter Msolla, akidai kuwa ana uwezo mdogo wa kufanya kazi na ndiyo maana Rais Jakaya Kikwete alimtema katika nafasi ya uwaziri.
Pia amemtaka Profesa Msolla kumuomba radhi kupitia gazeti (siyo NIPASHE) alilotumia kumdhalilisha, kumkejeli na kumvunjia heshima kwa kumuita mropokaji, vinginevyo atamchukulia hatua kali za kisheria.

 Lugola alitoa kauli hiyo jana mjini hapa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari ya Bunge.

Alisema anamshangaa Profesa Msola kwa kutokuwa na uelewa wa kutosha juu ya utendaji wake wa kazi jambo ambalo ni hatari kwa viongozi wa nchi.

Lugola alisema kitendo cha Profesa Msolla kumwita mropokaji siyo cha kiungwana na inaonyesha wazi kuwa ana ufahamu mdogo wa utendaji wa kazi.

“Inashangaza kuona kuwa hoja iliyomfanya ateuliwe kuwa mwenyekiti wa kamati hiyo iliwasilishwa na mimi bungeni. Lakini zaidi alipendekeza mwenyewe kuundwa kwa kamati na baadaye akawa mwenyekiti. Sasa ninachoshangazwa ni nini kinamuwasha hadi aanze kunishambulia?” alihoji Lugola.

Aliongeza: “Ushauri wangu kwa Profesa Msolla…kwanza ajipime, ajitafakari na achukuwe hatua ya kufanya kazi aliyopewa badala ya kukurupuka na kuanzisha malumbano,” alisema Lugola.

Alipotafutwa Professa Msolla kujibu tuhuma hizo jana, alisema kuwa alikuwa katika kikao.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa