Mikoani: Wananchi katika mikoa mbalimbali
nchini wameshangilia kung’olewa kwa mawaziri wanne, yakiwa ni matokeo ya
uchunguzi wa Bunge kuhusu Operesheni Tokomeza Ujangili.
Diwani wa Nyanungu, wilayani Tarime Mkoa wa Mara,
Samson Mang’enyi alisema operesheni hiyo ilifanywa kwa uonevu na
kuwaathiri wananchi wanaoishi pembezoni mwa Hifadhi ya Serengeti.
Mang’enyi alidai kuwa askari wa wanyama pori
wamekuwa wakiwapiga risasi raia na mifugo na kwamba wakati mwingine
wamekuwa wakiwafanyia vitendo vya kinyama kina mama na watoto ambao
walikuwa wakiingia katika Bonde la Nyanungu kuokota kuni.
“Miaka yote hapa kijijini tulikuwa tunategemea
Bonde la Nyanungu katika kulishia mifugo yetu, kulima na kina mama na
watoto kuokota kuni, lakini baada ya kutangazwa Operesheni Tokomeza, kwa
kweli hii nchi haina ubinadamu kwa baadhi ya watu,” alisema diwani
huyo.
Mkazi mwingine wa kata hiyo, Caro Chacha alisema
afya yake kwa sasa inazidi kuzorota baada ya kuchapwa viboko visivyo na
idadi na baadhi ya askari wanyama pori wa Hifadhi ya Serengeti (Senapa)
alipokuwa akiokota kuni katika Bonde la Nyanungu.
“Kwa kweli kipigo nilichokipata sitakisahau katika
maisha yangu. Nilikuwa nanyonyesha lakini nilishindwa hata kunyonyesha
mtoto, hata namna ya kujisaidia haja ndogo nilishindwa. Ila Mungu ni
mkubwa,” alisema na kuongeza:
“Askari hao walifikia hatua na kutuvua nguo zote,
tukabakia uchi wa mnyama kama tulivyozaliwa, jamani inauma sana kwani
pale walikuwapo watoto, walitufanyia vitendo vya ajabu sana. Walitaka
hata kutubaka ila walishindwa baada ya kuona tumeishiwa nguvu kwa mateso
ya muda mrefu.”
Ruvuma
Mkoani Ruvuma, wananchi wamekuwa na maoni
yanayokinzana, baadhi wamepongeza uamuzi wa Bunge na baadaye Serikali,
wakati wengine wameeleza kusikitishwa.
Mkazi wa Tunduru, Ajiri Omary Kalolo alisema
anaunga mkono uamuzi wa mawaziri kuondolewa madarakani akisema naye ni
mmoja wa watu walioteswa na askari waliohusika na Operesheni Tokomeza
Ujangili.
Kalolo alisema mbali na mateso aliyopata, aliwekwa mahabusu, kunyang’anywa fedha na kushinda njaa.
“Ninaunga mkono kung’olewa mawaziri wenye dhamana.
Hili ni funzo, kwani nchi ingekufumbua macho tatizo hili tungeweza
kufika pabaya zaidi ingawa najua wapo askari ambao wametesa wananchi kwa
matakwa yao na hawakutumwa kufanya hivyo, tunaiomba Serikali
iwachukulie hatua zaidi,” alisema.
Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Ruvuma,
Andrew Kuchonjoma ambaye pia alikamatwa na kuwekwa mahabusu kwa siku
tatu kwa kosa la kukutwa na mbao, alielezea kusikitishwa kwake na
kung’olewa kwa mawaziri kwa makosa yaliyofanywa na watendaji waliopo
chini yao.
Alisema hatua ya mawaziri kung’oka haitoshi badala
yake akataka Serikali iwachukulie hatua askari wote waliofanya vitendo
vya ukatili.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment