Home » » Miradi ya maendeleo 503 yatekelezwa Mara

Miradi ya maendeleo 503 yatekelezwa Mara

Jumla ya miradi 503 ya DASIP imetekelezwa na wawekezaji katika sekta ya kilimo katika halmashauri za Mkoa wa Mara kwa kushirikiana na wananchi, ambapo miradi 429 imekamilika na miradi 373 ndiyo inayotumika.
Hayo yalibainishwa jana na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mara ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Rorya, Elias Goroi,kwenye Warsha ya uendeshaji wa masoko ya bidhaa za kilimo iliyofanyika katika ukumbi wa uwekezaji uliopo ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Goroi alieleza kuwa DASIP imejitahidi kujenga miradi ya kijamii yakiwemo majosho 52 ya kuogeshea mifugo,malambo 54,maghala manne ya kuhifadhi mazao, masoko 11,barabara zenye urefu zaidi ya kilometa 50 na ujenzi wa soko la kimkakati katika Wilaya ya Tarime.
Nyingine ni ujenzi wa skimu za umwagiliaji katika halmashauri ya Bunda,Serengeti,Musoma na Rorya. Aidha, mradi wa DASIP umesambaza power tiller 51, mashine 77 za kukoboa na kusaga nafaka na majembe ya kukokotwa na ng'ombe 76 ambayo yameendelea kuboresha sekta ya kilimo katika wilaya hiyo.
Akichangia hoja, mkuu huyo alisema umefika muda wa Watanzania kuwa na masoko huria badala ya kuendelea kuwauzia wa nchi jirani.
ìWatanzania tumekuwa na tabia ya kudharau malighafi zinazozalishwa hapa nchini kwetu na kukimbilia bidhaa zinazotoka nje, hivyo kama hatutabadilika sisi wenyewe na kupenda bidhaa zetu tutaendelea kulalamika kila siku kuwa bidhaa zetu haziuzwi nje," alisema Mkuu wa Wilaya ya Tarime, John Henjewelle.
Henjewelle aliwaonya wakulima wanaouza mazao ya chakula yakiwa mashambani kuacha tabia hiyo mara moja kwa kuwa wanasababisha mapato kukosekana hasa kwa wale wanaonunua hivyo aliziagiza halmashauri kusimamia kikamilifu na kuweka sheria ndogo ili kudhibiti tatizo hilo.
Ofisa mafunzo wa Mradi wa DASIP na uwekezaji katika sekta ya kilimo wilayani, Julius Sonoko, alisema kuwa mojawapo ya changamoto ziliziowakwamisha ni kutokamilika kikamilifu kwa mradi huo ni ujenzi wa skimu za umwagiliaji za Nyakunguru wilayani Tarime na Kabanga Wilaya ya Kasulu ambazo hazijatekelezwa kutokana na migogoro ya mipaka na ardhi iliyopo kwa muda mrefu.

Chanzo;Majira

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa