WANANCHI wa kijiji
cha Majimoto, katika wilaya ya Serengeti, mkoani Mara, wamefurahishwa na
kitendo cha waziri wa nishati na madini Sospeter Muhongo kwa kuwatembelea na
kusikiliza kero zao mbalimbali zinazowakabili.
Wakiongozwa na
mwenyekiti wa kijiji hicho Bw. Johannet Masirori, wananchi hao wameiambia Radio
Free Africa, kuwa wiki iliyokwisha waziri huyo aliwatembelea, kwa ajili ya
kusikiliza kero zao mbalimbali ili ziweze kupatiwa ufumbuzi.
Wamezitaja kero hizo
kuwa ni pamoja na kero wanayodai walinyang’anywa ardhi yao na kampuni moja ya
Bismark iliyoingia katika eneo hilo kwa ajili ya utafiti wa madini aina ya
dhahabu.
Bw. Masirori amesema
kuwa baadaye kampuni hiyo mwaka 2006 ilianza uchimbaji wa dhahabu katika eneo
hilo bila kupewa na serikali ya kijiji na kwamba sasa imeweka uzio na kutaka
kuwahamisha wananchi kwa nguvu walioko katika eneo hilo.
Amesema kuwa mgogoro
huo ni mkubwa na ni wa siku nyingi, kwani wananchi wamegoma kwa sababu hawawezi
kuhamishwa bila ya kupewa fidia.
Ameongeza kuwa baada
ya waziri kuwatembelea na kusikia kero hiyo, alimwagiza kamishina wa kanda ya
ziwa kushughulikia malalamiko hayo, ikiwa ni pamoja na wananchi kulipwa fidia.
Wananchi hao wamesema
kuwa kitendo cha waziri Mhongo kuwatembelea na kusikiliza kero zao, ikiwemo na
ya kuukosa umeme ni faraja kubwa sana kwamba serikali inasikiliza kilio cha
wananchi wake.
Hata hivyo kampuni
hiyo imekuwa ikidai kuwa eneo hilo walilipata baada ya kupewa vibali na
serikali tangu mwaka 1991.
0 comments:
Post a Comment