WAJASIRIAMALI walioshiriki maonesho ya bidhaa katika Kanda ya Ziwa
wamelipongeza Shirika la Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO) makao makuu kwa
kuandaa maonyesho hayo ambayo yamewasaidia katika kutangaza bidhaa zao
sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti katika siku ya kilele
cha maonesho hayo yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi
Mkendo, Manispaa ya Musoma, Mkoa wa Mara, wamesema kuwa kumekuwepo na
mabadiliko ya mauzo katika siku hizo nne za maonesho hayo kuanzia
Novemba 29 hadi Desemba 2, mwaka huu tofauti na siku nyingine.
Wakitoa shukurani kwa uongozi wa Mkoa wa Mara na viongozi wote wa
Kanda ya Ziwa na makao makuu kwa kufanikisha zoezi hilo, wajasiriamali
hao walisema kuwa SIDO imekuwa ikiwakutanisha kwa pamoja wajasiriamali
wakubwa na wadogo hali inayowasaidia katika kubadilishana uzoefu wa
kazi na kuongeza ujuzi zaidi na kikubwa zaidi ni kuwasaidia
wajasiriamali wadogo kukua na kutangaza bidhaa zao.
“Hapa tunakutana na wajasiriamali mbalimbali kutoka ndani na nje ya
nchi. Mfano hawa wajasiriamali kutoka Nairobi, Kenya wanatupa hamasa
sisi Watanzania zaidi katika kuongeza juhudi ya kuzalisha kwa kuwa
tayari tunajua kuwa hata sisi bidhaa zetu tutaenda kuuza nje ya nchi,
hasa tunapokuwa tunashiriki maonesho kama haya ambayo huko Kenya wao
wanayaita JUA KALI,” alisema mmoja wa washirki kutoka Kagera.
Mbali na maonesho ya bidhaa mbalimbali zilizooneshwa katika maonesho
hayo, zaidi kilichowavutia watu wengi ni kichwa cha mtu kilichokuwa
kikiongea ambapo kukiona ilikuwa inakugharimu kulipia shilingi 1,000
kama unataka kuzungumza nacho na shilingi 500 kukiona tu bila kufanya
mazungumzo nacho.
“Kwa ujumla maonesho yalikuwa mazuri, tumeuza sana kiasi ambacho
hatukutarajia kabisa kulingana na sifa ya Mkoa wa Mara tunavyoisikia
kutokana na taarifa mbalimbali, lakini kumbe Mara ni mkoa mzuri sana,
watu wanafanya kazi kweli, tumejionea wenyewe,” alisema FANA Soap
muuzaji wa sabuni za Kigoma.
Nae Meneja wa SIDO Mkoa wa Mara, Frida Mungulu aliipongeza timu ya
SIDO Mara na SIDO Kanda ya Ziwa kwa kushiriki kikamilifu tangu siku ya
maonesho hadi kilele na kuwaomba waendelee na ushirkiano huohuo.
Akifunga maonesho hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, John
Gabriel Tuppa, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Jackson Msome alisema kuwa
uzoefu huo waliobadilishana katika maonesho hayo waendelee kuutumia
ili kuleta ufanisi katika bidhaa zao na wawe tayari kutumia fursa
zinazopatikana bila kurudi nyuma.
Chanzo;Tanzaia Daima
0 comments:
Post a Comment