SHIRIKA la umma la Hifadhi ya Taifa Tanzania (TANAPA), limetoa
mabati 6000, kwa ajili ya kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo
katika vijiji vinavyozunguka hifadhi za taifa.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Kaimu Mkurugenzi wa TANAPA, William
Mwakilemo, wakati akizungumza kwenye semina ya mafunzo ya siku sita kwa
wanahabari kuhusiana na ujirani mwema.
Mwakilemo ambaye pia ni Mhifadhi Mkuu wa TANAPA, alisema msaada huo
wa mabati umelenga kuchochea upatikanaji wa maendeleo ya jamii ya
vijijini.
Katika semina hiyo ya mafunzo iliyowashirikisha pia viongozi wa vijiji
na kimila, alisema msaada huo ulisaidia ujenzi wa shule, zahanati,
vituo mbalimbali vya polisi na miradi mingine iliyolengwa kwa mujibu wa
mahitaji halisi.
“Katika utekelezaji wa sera za ujirani mwema, TANAPA tumeweza kutoa
msaada wa mabati 600 kwa vijiji vinavyozunguka hifadhi za taifa. Mabati
haya yamesaidia ujenzi wa vituo vya polisi, shule na miradi mingine
kulingana na mahitaji,” alisema Mwakilemo.
Akizungumzia ujangili, alisema haupaswi kufumbiwa macho na kusema
jamii ina wajibu wa kutoa taarifa dhidi ya watu wanaojihusisha nao.
Alisema majangili wamo ndani ya jamii hivyo wananchi lazima washiriki
kupambana na kutoa taarifa kwa vyombo vya dola ili wakamatwe.
Aliiomba jamii kuheshimu sheria za nchi kwa kutoingia ndani ya
hifadhi za taifa kwa ajili ya malisho ya mifugo au kufanya shughuli
zozote bila kibali cha serikali.
Baadhi ya washiriki wa semina hiyo, walilalamikia kitendo cha askari
wa TANAPA kuipiga risasi mifugo na kuiua pindi inapoingia kwenye
hifadhi kwa bahati mbaya.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment