WAJUMBE wa baraza la mamlaka ya mji
mdogo wa Bunda, mkoani Mara, wamelalamikia kitendo cha halmashaurui ya wilaya
hiyo, kushindwa kulipia karo ya wanafunzi wanaoishi katika mazingira
magumu zaidi ya 70 kila mwaka na kusababisha wanafunzi hao kunyimwa vyeti vya
kumaliza kidato cha nne.
Wajumbe hao ambao ni wenyeviti wa
vitongoji katika mji huo, wamelalamikia kitendo hicho jana kwenye kikao cha
bajeti ya mwaka wa fedha 2014/2015, kilichofanyika mjini Bunda.
Wakiongozwa na mwenyekiti wa mamlaka ya
mji mdogo wa Bunda, Bw. Pastory Ncheye, wamesema kuwa mwaka wa fedha wa
2011/2012 na mwaka wa fedha wa 2012/2013, walipitisha bajeti kwamba watoto
zaidi ya 70 hadi 80, wanaosoma sekondari wawe wanalipiwa karo na mamlaka hiyo,
ambapo kila mtoto alipaswa kulipiwa sh. 20,000 kwa mwaka.
Wamesema kuwa pamoja na kupitisha
bajeti hiyo watoto hao hawajawahi kulipiwa karo hiyo na kusababisha kunyimwa
vyeti baada ya kumaliza kidato cha nne.
Wameongeza kuwa kwenye makaburasha ya
mamlaka hiyo fedha za kulipia wanafunzi hao zimekuwa zikitengwa, lakini cha
ajabu katika shule wanazosoma watoto hao, ikiwemo ya Dk. Nchimbi, karo hiyo
haijawahi kulipwa kwa vipindi vyote hivyo.
Kufuatia hali hiyo wamemtaka mkurugenzi
mtendaji wa halmashauri hiyo, Bw. Simoni Mayeye, kushughulikia kero hiyo ili
wanafunzi hao waweze kulipiwa karo yao.
Mkurugenzi huyo ameahidi
kulishughulikia suala hilo, kwa ajili ya kuondoa kero hiyo.
Mamla ya mji mdogo wa Bunda imepitisha
bajeti ya mwaka wa fedha wa 2014/2015, ambapo imekadiria kukusanya na kutumia
kiasi cha shilingi 423,955,200, makadirio ambayo ni chini ikilinganishwa na
mwaka wa fedha wa 2013/2014 kwani walikuwa wamekadiria kukushanya jumla ya sh.
595,080,000.
0 comments:
Post a Comment