WATU watano wameuawa kikatili kwa kuchinjwa, kukatwa mapanga katika
mfululizo wa matukio ya mauaji ya kinyama yanayoendelea kutokea katika
wilaya za Musoma, Butiama na Rorya mkoani Mara.
Kibaya zaidi, mauaji hayo ambayo yameendelea kutokea mfululizo ndani
ya wiki moja, yamekuwa yakiwalenga zaidi wanawake wanapokuwa mashambani
na wakati mwingine kuvamiwa majumbani mwao.
Mauaji ya kwanza yametokea hivi karibuni katika Kijiji cha Mkirira,
Kata ya Nyegina wilayani Butiama baada ya mwanamke mmoja kuuawa akiwa
shambani kwake kisha wauaji kuchimba shimo fupi na kuufukia mwili wake.
Mauaji hayo yameibua hofu kubwa kwa wananchi hasa wanawake katika
kijiji hicho kutokana na mfululizo wa mauaji ya aina hiyo ambapo hadi
sasa wanawake wanne kati ya watu watano, wameuawa kwa kukatwa mapanga
na kuchinjwa kama kuku.
Mauaji ya juzi ya mwanamke aliyejulikana kwa jina la Mkaguru Magee,
yamesababisha wanawake wa kijiji hicho kujifungia ndani na
kushindwa kwenda kwenye shughuli za kilimo kwa kuogopa kuuawa.
Siku moja baada ya mama huyo kuuawa kinyama, yakaibuka mauaji ya
Mwenyekiti wa CCM Tawi la Nyakato kwa Sanane katika Manispaa ya Musoma
mkoani Mara, Shaban Wambura aliyeuawa kwa kunyongwa kisha kutobolewa
macho yote.
Baada ya mauaji hayo ya kikatili, wauaji walichukua mwili wa marehemu
na kwenda kuutupa katika majaruba ya mpunga maeneo ya Shule ya
Msingi Mshikamano, mjini Musoma.
Baadhi ya watu wakiwemo watoto wa marehemu ambao walifika
kushuhudia mwili kabla ya kuchukuliwa na polisi, walisema kabla ya
kifo chake mwenyekiti huyo alitoka nyumbani kwenda matembezini ambako
hakuweza kurudi hadi mwili wake ulivyokutwa umetupwa katika eneo hilo.
Katika tukio jingine watu wasiojulikana wamewaua kikatili kwa
kuwakata mapanga mama mmoja na kijana wake ambaye alikuwa amefaulu
kujiunga na kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Suba.
Mama na mwanaye huyo, walivamiwa na wauaji hao wakati wakipata
chakula cha usiku nyumbani kwao katika Kijiji cha Komuge wilayani
Rorya mkoani Mara.
Mauaji ya mama huyo, Matinde Waryuba (46), yamefanyika saa mbili
usiku katika kijiji hicho ambapo aliuawa kwa kuchinjwa na kukatwakatwa
mapanga katika sehemu mbalimbali za mwili wake, huku mtoto wake wa
mwisho, Thobias Waryuba (14), naye akiuawa kwa kukatwa mapanga sehemu
za shingo na mabegani.
Ndugu wa marehemu, Prisca Misana, alisema hadi sasa familia
haijatambua sababu za mauaji hayo ya kikatili huku wakitoa wito kwa
serikali kuwasaka wauaji hao katika kuondoa hali ya kulipizana visasi.
Polisi mjini Musoma imethibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kwamba
hadi sasa uchunguzi wa kina unafanywa kujua chanzo chake na kubaini
wauaji ili waweze kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Kwa upande wao, baadhi ya wazee wa mila ambao wamekutana muda mfupi
baada ya kutokea kwa mauaji hayo, wamelaani vikali vitendo hivyo vya
kikatili, huku wakitaka serikali kupitia vyombo vya dola kufanya
uchunguzi wa kina kuhakikisha wauaji hao wanakamatwa na kufikishwa
katika vyombo vya sheria.
Miili ya marehemu hao imechukuliwa na polisi wa Wilaya ya Rorya kwa
uchunguzi zaidi na kisha kuhifadhiwa katika chumba cha maiti cha
hospitali ya serikali ya Mkoa wa Mara mjini Musoma na inatarajia
kuzikwa kesho.
Wakizungumza baada wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama
wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Angelina Mabula, wananchi
wa kijiji hicho wameitaka serikali kuchukua hatua za haraka
kumaliza mauaji hayo, kwani hivi sasa hakuna mwanamke
anayekwenda shambani bila ya ulinzi.
“Shughuli za kilimo zimesimama, wanawake wote wameogopa kwenda
shambani, mfano mimi ndio mtafutaji, lakini leo mke wangu ameniambia
nimpeleke shamba kutokana na hofu hiyo, sasa tutaishi vipi?” alihoji
Jumanne Magafu.
Kwa upande wake, mkazi mmoja ya kijiji hicho, Maria Majura, aliiomba
serikali licha ya kufanya doria za usiku, pia polisi wahusike kufanya
doria za mchana ili kukabiliana na mauaji hayo ya kikatili.
Kwa upande wao, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ngazi
ya mkoa na taifa, wakiongozwa na Katibu wa UWT Taifa, Amin Makiragi,
wamelaani mauaji hayo ya kikatili huku wakitaka vyombo vya
dola kuwasaka wauaji hao na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
Mkuu wa Operesheni wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara, Oudax
Majaliwa, ameomba jamii kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi
na usalama kufanikisha kukamatwa kwa wauaji hao.
Mtoto na mjukuu wa Meja Jenerali Marwa wauawa
Wakati huo huo, Mwandishi Igenga Mtatiro anaripoti kuwa aliyekuwa
askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na aliyehitimu mafunzo
ya ukomandoo wa jeshi hilo, Zacharia Chacha Marwa ambaye ni mtoto wa
Marehemu Meja Jenerali, Mwita Marwa, ameuawa kwa kupigwa risasi usiku wa
kuamkia jana.
Mwingine aliyeuawa katika tukio hilo ni mjukuu wa Meja Jenerali
Marwa, Erick Lucas Mohabe (24) ambaye pia aliuawa kwa kushambuliwa na
risasi katika tukio hilo hilo.
Mauaji hayo yalitokea katika Kijiji cha Mogabiri, Kata ya Ketare, Tarafa ya Inchage, Wilaya ya Tarime mkoani Mara.
Kwa mjibu wa mdogo wa marehemu, aliyejulikana kwa jina la Joseph
Marwa, waliouawa ni ndugu zake na hadi sasa hawajui chanzo cha mauaji
yao.
Kamanda wa Polisi Tarime na Rorya, Justus Kamugisha, alithibitisha
kutokea tukio hilo na kwamba askari walikuwa wanaendesha msako mkali
kuwabaini wahusika hao.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment