Home » » Mbegu mbovu zatengeneza mafuta ya kula Mara

Mbegu mbovu zatengeneza mafuta ya kula Mara

Meneja wa Kiwanda cha Bundaa, Roharl Parmar (kushoto) akiwa na Kaimu Afisa Shughuli wa kiwanda hicho, Paul Aaron wakati alipohojiwa na gazeti hili ofisi kwake

Bunda. Baadhi ya viwanda Mikoa ya Mara na Mwanza vinadaiwa kutumia mbegu za pamba zilizooza kwa ajili ya kuzalisha mafuta ya kula, hali ambayo inahatarisha afya za watumiaji wa mafuta hayo.
Uchunguzi uliofanywa gazeti hili ulibaini kuwa baadhi ya viwanda vya kuzalisha mafuta vimekuwa vikinunua mbegu hizo kwa bei nafuu kwa madai ya kuzitumia kutengenezea mashudu (chakula cha mifugo) na kuchomea
`boiler’ (chombo cha kuchemshia malighafi ya mafuta), lakini zimekuwa zikitumika kinyume.
Badala yake zimekuwa zikitumika kukamua mafuta ambayo kutokana na kuwa machafu, huchanganywa na mafuta mengine masafi kisha kuingizwa sokoni.
Uchunguzi ulibaini kuwa mchezo huo umekuwa ukifanyika kwa muda mrefu, kabla ya kugunduliwa na wataalamu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA), Kanda ya Ziwa, kutokana na kuwapo kwa malalamiko mengi kutoka kwa walaji.
Imebainika kuwa TFDA walifanya ukaguzi wa kushtukiza katika Viwanda vya Bundaa Oil Mill kilichoko wilayani Bunda mkoani Mara na Brichand Oil Mill Ltd kilichopo jijini Mwanza kutokana na kudaiwa kujihusisha na mchezo huo.
Meneja wa TFDA, Kanda ya Ziwa, Moses Mbambe alisema: “Malalamiko ya walaji yalitusukuma kufanya msako wa kustukiza kwenye Kiwanda cha Brichand Oil Mill Ltd…Wakakiri kuuza mbegu zilizooza kwa Kampuni ya Bundaa Oil Mill Ltd na katika kufuatilia ndipo tulibaini ukiukwaji huo wa sheria huo,” alisema Mbambe.
Mbambe alisema uongozi wa Brichand Oil Mill Ltd ulisema kuwa mbegu hizo waliwapa Bundaa Oil Mill Ltd kwa madhumuni ya kutengeneza mashudu na siyo vinginevyo, lakini TFDA katika ukaguzi wao walibaini mbegu hizo zilitumika kwa ajili ya kuzalisha mafuta.
Mkaguzi wa Vyakula katika Mamlaka ya Mji mdogo wa Bunda, Mafuru Madaraka alikiri kiwanda hicho kuhusika kutumia mbegu zilizooza kutengeneza mafuta ya pamba.
“Ni kweli tulivamia tukiwa na wataalamu wa TFDA na kukuta wakizalisha mafuta kwa kutumia mbegu zilizooza…mafuta mengine yakiwa yameshaingia sokoni na mengine yakiwa yamehifadhiwa stooni,” alisema Madaraka.
Alisema mbegu hizo zilichukuliwa na kuamriwa kuteketezwa chini ya usimamizi wao na TFDA, huku uongozi wa kiwanda hicho ukidai kuwa mbegu hizo waliuziwa na Kiwanda cha Brichand Oil Mill Ltd.
“Inaonekana ni mtandao licha ya kudai waliwauzia mbegu zilizooza lakini kulikuwa na ndoo za Kampuni ya Brichand Oil Mill Ltd…Ina maana mafuta yaliyokuwa yanazalishwa ilikuwa kampuni hiyo iyachukue…Hatujui wanayaingizaje sokoni yakiwa hivyo,” alisema Madaraka.

Viongozi wa viwanda
Meneja wa Bundaa Oil Mill Ltd, Rohan Parmar alikiri kukamatwa wakisaga mbegu chafu na kudai kwamba walipewa mbegu hizo na Kampuni Brichand Oil Mill Ltd.
Alipotakiwa kufafanua sababu za kukubali kupokea mbegu chafu wakati wakijua sheria hairuhusu alisema: “Kwanza muda huo nilikuwa Igunga sijui mambo mengi…Sisi tumepata shida sana tumekosa mbegu sasa tumesimamisha uzalishaji ….Hayo mengine sipendi kuyasemea.”
Baada ya gazeti hili kumbana kwamba alikuwapo kama msimamizi wakati TFDA walipowakamata, aling’aka akisema: “Sasa wewe unataka mambo mengi ya nini…Walikamata mbegu wakachoma ...Sisi sasa tumefunga kiwanda…Unataka nini tena…Mimi siwezi kusema mpaka mwanasheria wa kampuni awepo.”
Alipotakiwa kumtaja mwanasheria ili afuatwe kutoa ufafanuzi, Maramar alikataa akisema: “Siwezi kusema majina, wala alipo, wala namba…Wewe ‘tafuta’ sisi baada ya wiki moja.”
Jitihada za gazeti hili ziliwezesha kupatikana kwa Mwanasheria wa Kampuni, Denis Masami ambaye alipoulizwa kuhusu uzalishaji wa mafuta kwa kutumia mbegu zilizooza aliomba apewe nafasi ya kufuatilia kwa kuwa wakati wanakamatwa na TFDA alikuwa bado hajaajiriwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Brichand Oil Mill Ltd, Mohammed Sharif alikiri kiwanda chake kuwauzia Bundaa Oil Mill Ltd, mbegu chafu lakini kwa kwa ajili ya kusafisha `Boiler’.
“Walichukua kwa makubaliano kuwa wanakwenda kusafisha mashudu ili yawe meupe badala ya mafuta…Maana wana mtambo usio wa kawaida una uwezo wa kuchanganya mbegu zilizooza na safi ukasaga bila matatizo…Mitambo mingine haiwezi kufanya hivyo,” alisema.
Wasemavyo wananchi
Uchunguzi umebaini kuwa baadhi ya wananchi walilalamikia mafuta yanayotokana na mbegu hizo, lakini kwa upande mwingine yalikuwa yakipendwa na wakaanga samaki kutokana na kuuzwa kwa bei rahisi ikilinganishwa na mafuta ya aina nyingine.
Mkazi wa Kijiji cha Migungani, Bunda ambao Kichere Gikaro (60 alisema kulikuwa na malalamiko mengi kutoka kwa watumiaji wa mafuta yalitoka katika Kiwanda cha Bundaa Oil Mill Ltd.
“Hapa kwetu sisi ndio tulitakiwa kuwa wateja wakubwa kwa kuwa kiwanda kiko hapa……lakini kutokana na malalamiko ya watumiaji wengi kuhusu ubora wake, tulilazimika kwenda kununua mafuta mengine mjini, malalamiko

haya yaliwafikia watu wa afya, lakini hatukupata majibu,” alisema Gikaro.
Muuzaji wa mafuta katika Soko Kuu la Bunda Mjini aliyejitambulisha kwa jina la Nashon alikiri kwamba alikuwa na wakati mgumu kuuza mafuta hayo kutokana na kulalamikiwa kwamba yalikuwa na uchafu pia harufu mbaya.
“Ilikuwa shida kweli maana licha ya kwamba bei yake iko chini lakini soko lake ni gumu sana, kama unavyojua sisi wafanyabiashara tunataka unaponunua mali basi itoke ili pesa yako izunguke,” alisema Nashon.
Naye Sundi Juma ambaye ni muuza samaki stendi Kuu ya Bunda, alisema yeye anayapenda mafuta hayo kutokana na ukweli kwamba ni mazito hivyo hayaishi haraka anapokuwa akikaanga samaki wake.
“Kwanza mafuta haya ni bei ni nafuu…Ni mazito, ukinunua kidogo unakaanga samaki wengi…unatumia gharama ndogo, ingawa wateja wanalalamika harufu hasa samaki wakila lakini kwetu ni nafuu…Maana mafuta mengine bei iko juu na ni mepesi,”alisema Juma.
Alisema bei ya mafuta hayo yanayozalishwa na Bundaa Oil Mill Ltd ni Sh 1,400 kwa lita moja, ikilinganishwa na mafuta aya aina nyingine ambayo yanauzwa Sh2,000 kwa kiasi hicho.
“Ukinunua mafuta ya bei kubwa unalazimika kuuza samaki pia kwa bei kubwa, wakaanga samaki hatuko tayari kununua mafuta ya bei ya juu…Kwa kuwa ukinunua wewe mwenzio anachukua ya bei ya chini, anauza samaki bei nzuri, wako wanabaki,” alisema.
Juma alikiri kuwapo kwa watu wanaolalamika kujisikia vibaya hasa wanapokuwa wanakaanga samaki kutokana na mvuke unaotokana na mafuta hayo kubadili hali ya hewa na kuwa nzito.
Madhara kiafya
Mmoja wa maofisa wa TFDA, Kanda ya Ziwa ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe kutokana na kutokuwa msemaji wa taasisi hiyo, alisema miongoni mwa madhara yanayoweza kumpata mtumiaji ni saratani.
“Uzalishaji wa mafuta hayo hutumia kemikali aina ya caustic soda ambayo kisheria lazima isimamiwe na mtaalamu, lakini hata mkemia hawakuwa naye…Wanazalisha mafuta kwa mbegu zilizooza…Wanawalisha watu vitu visivyo stahiki…madhara yake ni makubwa kiafya,”alisema.
Mfamasia na mmiliki wa zahanati binafsi wilayani Serengeti Mkoa wa Mara, Thomas Burito alisema madhara kwa watumiaji wa mafuta hayo ni makubwa kwa kuwa husababisha mishipa kuziba na matokeo yake ni watumiaji kuugua saratani na figo.
“Matumizi ya mafuta kama hayo ni hatari kwa maisha ya walaji, kiafya wanaathirika polepole na wengi hupata kansa, ugonjwa ya moyo, figo na hayo ni magonjwa hatari na mwisho kama hakuchukua hatua haraka ni vifo,” alisema Burito.
Ofisa Afya wa Wilaya Bunda, Fadhili Kinyogoli alisema matatizo ya kuzalisha mali zisizo na kiwango na kuziingiza sokoni ni kubwa kutokana na wananchi ambao ni walaji kutokutoa taarifa kwa wakati ili hatua ziweze kuchukuliwa.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa