Home » » MWENYEKITI CCM AMTAKA DC AMWOMBE RADHI

MWENYEKITI CCM AMTAKA DC AMWOMBE RADHI

Musoma. Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Rorya mkoani Mara, Samwel Kiboye, amempa siku saba Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Elias Goloi kumwomba radhi kwa madai ya kusema kuwa anaweza kutumia ngumi na mateke kumwadhibu yeye na mbunge wa jimbo hilo kwa kuwatuhumu wanahimiza wananchi kugomea kulipa ushuru.
Alisema endapo mkuu huyo wa wilaya atashindwa kufanya hivyo, atalazimika kuitisha maandamano makubwa ya wilaya kwa ajili ya kushinikiza Rais Jakaya Kikwete, kumwondoa kiongozi huyo kwa madai amekuwa mzigo kwa chama chake huku akishindwa kutatua kero zinazowakabili wananchi wa wilaya hiyo.
Kauli ya kiongozi huyo wa CCM ambayo ameitoa kwa njia ya simu akiongea na gazeti hili, imekuja siku chache tu baada ya mkuu huyo wa wilaya Rorya akiwa katika Kikao cha Ushauri cha Mkoa (RCC) mjini hapa chini ya Uenyekiti wa Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Tupa kusema wilaya yake haiwezi kuongozwa kwa misingi ya utawala bora sasa bali atalazimika sasa kutumia ngumi na mateke ili kuwadhibiti wanasiasa hao.
“Mimi sipendi unafiki, mwenyekiti wangu wa chama tawala wilaya(Kiboye) na mbunge (Lameck Airo) wamekuwa wakirudisha nyuma maendeleo ya halmashauri kwa kuwazuia wananchi kulipa ushuru.Sasa nitaanza kutumia ngumi na mateke na wale watakaoshindwa kulipa ushuru lazima niwakamate na kuwapeleka mahabusu kisha wakafungwe ili wakajifunze adabu,” alisema DC Goloi.
Chanzo:Mwannchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa