Home » » UBADHIRIFU WAKIMBIZA WAFADHILI

UBADHIRIFU WAKIMBIZA WAFADHILI

Serengeti. Kamati ya Shirika la New Yearly Meeting la Marekani, imesitisha ufadhili wa wanafunzi wanaosoma elimu ya juu, vyuo mbalimbali na ujenzi wa nyumba za walimu shule ya msingi na sekondari Kisangura, wilayani Serengeti kutokana na jamii kutotoa ushirikiano.
Shirika hilo muda mrefu limekuwa kila mwaka likitoa ufadhili wa ujenzi wa nyumba za walimu, vyoo na matangi ya maji, kusomesha watoto yatima kupitia kamati ya Kanisa la Marafiki Kisangura na baadaye Shirika la Mugumu Children Foundation.
Hata hivyo, kumekuwa na taarifa za ubadhirifu ikiwamo baadhi ya miradi kutokutekelezwa.
Mkurugenzi wa Shirika la Zinduka, Maximillian Madoro alibainisha hayo wakati wa kutoa vifaa vya shule kwa wanafunzi 125 wa shule za msingi na sekondari Kisangura, kuwa ubadhirifu wa fedha umewakatisha tamaa.
“Kutokana na ubadhirifu huo walikuwa wameamua kusitisha kabisa… lakini tulipokutana nao tumewaeleza athari zake kwa watoto, wameomba Zinduka kusimamia kipindi hiki cha mpito,” alisema Madoro na kuongeza:
“Lakini wanafunzi wote waliokuwa wanapata ufadhili wa kulipiwa kidato cha tano, vyuo mbalimbali na ujenzi wamesitisha... maana fedha zinazotolewa hazifanyi kazi iliyokusudiwa.”
Madoro ambaye ni Diwani wa Kata ya Nyamswa, wilayani Bunda, alisema misaada hiyo waliyotoa yenye thamani ya Sh24 milioni inahusisha ukamilishaji choo cha wanafunzi.
Akizungumzia uamuzi huo,Mwakilishi wa kamati hiyo kutoka Marekani, Brian Singer alisema wamefikia uamuzi huo kutokana na michango yao ililenga kupunguza tatizo la watoto wa jamii hiyo kukosa elimu, lakini wazazi, walezi na wananchi hawatoi ushirikiano.
Singer alisema wana mpango wa kupeleka kompyuta kwenye shule hizo.
“Kwa sasa kuna mpango wa kuleta komputa kwa shule hizi mbili…tutawasainisha mikataba ili kuweza kuwabana wanaopokea,maana misaada mingi badala ya kwenda kwa walengwa inageuka ya watu wasiostahili….tutaleta kama wananchi watashiriki ujenzi wa vyumba vya kuhifadhia,”alisema.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa