UMEZUKA mvutano
mkubwa katika baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Bunda, mkoani
Mara, kuhusu mgawanyo wa fedha za miradi ya maendeleo, ambapo madiwani wa jimbo
la Mwibara wamelalamika kwamba jimbo la Bunda linatengewa fedha nyingi na
Mwibara kupewa kidogo.
Mvutano huo umetokea
jana kwenye kikao cha bajeti ya mwaka wa fedha wa 2014/2015 cha baraza hilo
kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri mjini Bunda, ambapo nusura bajeti
hiyo isipitishwe.
Katika kikao hicho
kilichokuwa chini ya mweyekiti wake Joseph Malimbe, baadhi ya madiwani wa kata
za jimbo la Mwibara walikataa kuipitisha bajeti hiyo kwa madai kuwa kuna
upendeleo wa fedha za ruzuku ya serikali na mfuko wa barabara.
Madiwani hao wamesema
kuwa hawako tayari kupitisha bajeti hiyo kwani fedha nyingi zimeelekezwa katika
jimbo la Bunda,kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
Diwani wa kata ya
Kisorya (CCM) Misana Jigwila na diwani wa kata ya Nansimo (CCM) Sabatho
Mafwimbo, waliwaongoza wenzao katika kulalamikia hali hiyo, huku madiwani wa
kata za jimbo la Bunda wakiwabeza kwamba bajeti hiyo imeshapitishwa na vikao
vya kamati.
Mvutano huo ulimfanya
mbunge wa Mwibara Kangi Lugola, kuingilia kati na kusema kuwa niwajibu wa
madiwani kuchangia bajeti hiyo kwani baraza hilo ndilo linaloipitisha na sio
vikao vya kamati za kudumu.
Hata hivyo kutokana
na mvutano huo, zilipigwa kura na waliosema ipitishwe wakashinda na ndipo
bajeti hiyo ikapitishwa, ambapo sh. bilioni 1.7 za ruzuku ya serikali
zimetengewa katika kata za jimbo la Bunda, huku Mwibara ikiambulia sh milioni
579 tu.
Aidha mfuko wa
barabara zimetengewa kilomita 151.5 zenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni 1.5
katika jimbo la Bunda, lakini Mwibara ni kilomita 72 tu zenye thamani ya zaidi
ya sh. milioni 956.
0 comments:
Post a Comment