Home » » Wanafunzi Marasibora wajisaidia vichakani

Wanafunzi Marasibora wajisaidia vichakani

WANAFUNZI wa Shule ya Msingi Marasibora iliyoppo Kata ya Kisumwa, wilayani Rorya, Mkoa wa Mara, wanajisaidia vichakani baada ya vyoo vya shule hiyo kuanguka.
Hatua hiyo inatokana na uongozi wa serikali ya kijiji kushindwa kujenga baada ya kudaiwa kutafuna fedha zilizotokana na mauzo ya viwanja 24 vyenye thamani ya sh milioni 2.4 na wananchi kugoma kufanya maendeleo ya kijiji hicho.
Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo, Ayuke Nyadelo alibainisha hayo alipozungumza na waandishi wa habari shuleni hapo.
Alisema matundu manne ya choo cha wasichana yanatumiwa na wanafunzi wote 588 baada ya choo cha wavulana chenye matundu manne kuanguka.
Nyadelo alikiri upungufu huo unachangia baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo kujisaidia katika vichaka vilivyopo karibu na shule hiyo, jambo alilosema  kuwa ni hatari kwa kugongwa na nyoka na kupatwa na magonjwa ya mlipuko kama kupindupindu.
Pia alisema zipo nyumba za walimu mbovu ambazo zinakaribia kuanguka, hali iliyofanya  baadhi ya walimu kukimbia wakihofia usalama wao.
Viongozi hao walipoulizwa juu ya tuhuma za kutafuna fedha, Mwenyekiti hakuwa tayari kuzungumza na waandishi wa habari kwa kile alichodai hana muda wa kikao cha kamati ya maendeleo kilichokuwa kikiendelea jana katika Shule ya Sekondari Kisumwa kilichoongozwa na diwani wa kata hiyo, Malaki Omolo.
Mtendaji wa kijiji hicho, Pilly Ntondo, alipotakiwa kutoa ufafanuzi alikanusha kutafuna mapato ya fedha za kijiji na kusema madai yaliyotolewa hayana uthibitisho wowote wa kisheria
Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa