WATU wawili wamefariki dunia kwa kupigwa risasi na watu
wanaosadikiwa kuwa majambazi baada ya kuvamia Tarafa ya Ingwe, Wilaya ya
Tarime, Mkoa wa Mara.
Kamanda wa Polisi Tarime na Rorya, Justus Kamugisha, aliwataja watu
waliouawa kuwa ni Muniko Koroso (23), mkazi wa Kijiji cha Keisangura,
Kata ya Nyamwaga na Matiko Mabura (39), mkazi wa Kijiji cha Mriba, Kata
ya Mriba.
Kamanda Kamugisha alisema watu hao walivamiwa saa 2 katika makazi yao
na watu wasiofahamika na kisha kuwapiga risasi na kutoweka
kusikojulikana.
Alisema katika tukio hilo Marwa Nyandege (34), mkazi wa Kijiji cha Mriba, alijeruhiwa kwa kupigwa risasi pajani na mguuni.
Katika tukio jingine, watu wanne wa Kijiji cha Bubombi, Kata ya
Bukura, wanahofiwa kufa maji baada ya kuzama walipokuwa wakivua samaki
katika Ziwa Victoria, baada ya mtumbwi wao kupigwa na dhoruba.
Ajali hiyo ilitokea Desemba 30 mwaka jana, saa 4 usiku.
Wanaohofiwa kufa maji ambao wanaendelea kutafutwa ni Kigocha Mahanga
(36), Kimune Masimba (47), Abdullah Twabare (70) na Mabere Nyamarege
(62).
Wakati huohuo, dereva wa pikipiki mkoani Iringa, amevunjika mguu na
abiria wake kujeruhiwa wakati wakisherehekea mwaka mpya 2014.
Ajali hiyo ilitokea juzi usiku ikiwa ni dakika 20 baada ya kuuaga mwaka 2013 na kuukaribisha mwaka 2014.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema dereva huyo akiwa katika mwendo
mkali waligongwa na gari T 397 AEZ lililokuwa limehama upande wake na
kuwaangusha.
Akizungumza kwa shida akiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Iringa, dereva huyo wa pikiki, Joseph Nyogele, alisema akiwa katika
harakati za kulikwepa gari hilo alijikuta akigongwa na kuvunjika mguu
wa kushoto huku abiria wake akipoteza fahamu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Ramadhan Mungi, alithibitisha
kutokea kwa ajali hiyo na kusema mbali na ajali hiyo waliuaga mwaka
2013 na kuukaribisha mwaka 2014 kwa amani na utulivu.
Ofisa Muunguzi wa zamu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Iringa, Eda Sanga, alisema dereva huyo wa pikipiki alivunjika mguu
wa kushoto na kwamba umekatwa na sasa hali yake inaendelea vizuri
huku abiria wake ametibiwa na kuruhusiwa.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment