Aweka wazi madudu ya serikali
Operesheni ya pili wakati wowote
Operesheni ya pili wakati wowote
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli.
Askari huyo ambaye jina lake tunalisitiri kwa sasa kwa sababu za kiusalama na taaluma, alizungumza na NIPASHE na kueleza kwa kina kinachoendelea nyuma ya pazia juu ya malipo yao, ikiwa ni siku moja tu baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli, kusema kwamba askari zaidi ya 2,000 kutoka vyombo vya ulinzi na usalama walioshiriki katika Operesheni Tokomeza Majangili awamu ya kwanza hawajalipwa fedha zao.
Juzi Lembeli alisema katika operesheni hiyo, serikali ilikuwa imetenga zaidi ya Sh. bilioni 3.5 kwa ajili ya kuitekeleza, lakini inashangaza kuambiwa kuwa askari waliohusika wanaendelea kusotea posho.
Jana askari huyo alisema kuwa serikali imekuwa ikiwapa ahadi za uongo kuhusiana na malipo ya fedha zao.
Askari huyo alisema Desemba 20, mwaka jana alipojiuzulu aliyekuwa waziri wa Maliasili na Mazingira, Balozi Khamis Kagasheki na wenzake watatu, Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na JKT), Dk. Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani ya Nchi) na Dk. David Mathayo David (Mifugo na Uvuvi) uteuzi wao kutenguliwa, ndipo walipoondoka katika maeneo ya operesheni na kuelekezwa waache akaunti zao za benki na namba za simu kwa ajili ya kuingiziwa malipo hayo.
Hata hivyo, askari huyo alisema hadi leo siku 46 hawajalipwa fedha hizo na kwamba kila siku wamekuwa wakipigwa kalenda kwa kuambiwa njoo kesho.
Alisema yeye na wenzake wa vyeo vya chini kila mmoja anadai Sh. 2,060,000.
Aliongeza kuwa operesheni hiyo licha ya kuwa na nia nzuri ya kutokomeza ujangili, lakini usimamizi haukuwa mzuri kutokana na mamlaka zote za utawala zilizohusika kukosa uratibu.
Alisema waliokuwa wanauliza juu ya haki zao kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), walielezwa kuwa wahusika ni Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
“Haikuwa rahisi kupata taaraifa muhimu juu ya haki zetu. Tulikuwa tunapata za juu juu kwenye posti (vituo vidogo) vilivyoanzishwa kwa ajili ya operesheni.
Alisisitiza kuwa posti hizo hazikuwa na mamlaka yoyote ya kiutendaji mbali tu ya kuwa ni sehemu ya kuratibu operesheni.
Juzi Lembeli alisisitiza kuwa: “Kusitishwa kwa operesheni hakukumaanisha ukomo wake kwa kuwa askari waliendelea kulinda usalama wa maeneo yale na katika kazi hiyo ambayo wameifanya kwa moyo mmoja mpaka sasa, walitakiwa kulipwa posho zao, jukumu ambalo limesahaulika. Kwa hiyo kamati, inaitaka serikali kuhakikisha kwamba inalipa posho inazodaiwa na askari waliohusika katika operesheni hiyo.”
Askari walioshiriki operesheni hiyo ni wanajeshi 480 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi 440, wamo pia askari 440 kutoka Kikosi dhidi ya Ujangili (KDU), askari wa Wanyamapori kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) na Usalama wa Taifa.
Wengine ni askari 99 kutoka Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) na askari Wanyamapori 51 kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).
TOKOMEZA KUANZA UPYA
Katika hatua nyingine Serikali jana ilietangaza rasmi kuanza upya kwa ‘Operesheni Tokomeza Majangili’ awamu ya pili muda wowote kuanzia sasa huku ikisisitiza kwamba itawakumba watu wote wanaojihusisha ujangili pamoja mitandao ya biashara za pembe za tembo na faru.
Akizungumza kwenye mkutano ulioikutanisha serikali, mabalozi wa nchi mbalimbali na taasisi za kimataifa, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alisema operesheni hiyo itafanyika kwa nguvu kuanzia porini, ofisini hadi majumbani.
Alisema serikali imefanya maandalizi ya kutosha kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa opereshehi hiyo baada ya kusitishwa Oktoba 31, mwaka jana kutokana na malalamiko ya kuwapo kwa vitendo vya ukatili, mateso, mauaji ya wananchi wasio na hatia pamoja na upotevu wa mali zikiwamo fedha na mifugo.
Aidha, Nyalandu alitaja maadui wakubwa watakaopambana nao katika operesheni hiyo ni watu wanaotumiwa kuua wanyamapori, wafadhili wa mitandao na pamoja na kuziomba nchi ambazo nyara hizo zinatoroshewa kusaidia kuzirudisha.
Hata hivyo, Nyalandu aliwaambia wajumbe wa mkutano huo kwamba katika zoezi hilo hakutakuwa na dosari zilizotokea awali, badala yake litafanyika kwa weledi na ufanisi.
“Serikali inatangaza kuanzia sasa zoezi la kuwatafuta majangili na wafadhili wa biashara ya pembe za tembo, tutaianza kwa kasi na nguvu kubwa, hakuna tutakayemuacha, tutawakamata majangili wote kuanzia porini, ofisini hata majumbani, hakuna sehemu watakayokimbilia,” alisema Nyalandu.
Hata hivyo, alikataa kutaja siku maalum ya kuanza kwa operesheni hiyo badala yake aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa ajili ya kuokoa nchi dhidi ya watu hao aliowaita hatari.
“Watu watambue tutaingia kwenye mapambano haya muhimu kwa ajili ya nchi yetu, watuunge mkono kuwatokomeza na hatimaye tuwe na wanyama kwa maslahi ya kizazi kijacho,” aliongeza.
Akizungumzia suala la askari wanaodai kutolipwa pesa zao kiasi cha Sh. bilioni 1.5 baada ya zoezi hilo kusitishwa, Waziri Nyalandu alithibitisha kuwako kwa deni hilo na aliahidi kulilipa.
Alisema wizara yake inafanya kazi ya kuhakiki deni hilo pamoja na kuhakikisha kwamba wale watakaolipwa siyo waliohusishwa na tuhuma ya ukatili, mateso na mauaji.
“Hakuna askari atakayeachwa bila kulipwa, lakini niweke wazi kwamba watu wote walifanya kazi kutokana na uzalendo wa nchi, hivyo malipo kama yapo ni kitu cha ziada tu,” alisema Waziri Nyalandu.
MKUTANO WA JANA
Mkutano huo uliosimamiwa na Shirika la maendeleo la Kimataifa (UNDP) ulijadili njia mbalimbali ya kukabiliana na ujangili nchini pamoja na kusaidia kubuni mikakati shirikishi ya kutokomeza vitendo hivyo ili kuokoa tembo wanauliwa kwa kasi katika hifadhi za Taifa na mapori ya akiba.
Mabalozi waliohudhuria ni kutoka Marekani, Uingereza, Ujerumani, Ufaransa, China, Japan na wawakilishi kutoka nchi zingine za Asia. Pia zimo Banki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika, Unesco na WFP.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment