WAFANYABIASHARA wa eneo la Sabasaba katika mji wa Tarime, mkoani
Mara, wamelalamikia kitendo cha kikatili kilichofanywa na mkurugenzi wa
halmashauri ya mji huo cha kubomoa vibanda vyao usiku bila
kuwataarifu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Tanzania Daima jana, baadhi ya
wafanyabiashara hao walieleza kusikitishwa na zoezi hilo kuendeshwa saa
8 usiku, hivyo kukosa nafasi ya kutoa mali zao.
Mmoja wa wafanyabiashara hao, Maluki Mdoye, aliyekuwa akifanya
biashara ya mgahawa, alieleza kushtushwa na kitendo hicho kwani alikuta
baadhi ya mali zake zikiwa nje na nyingine zenye thamani ya sh zaidi
ya milioni nane zikiwa hazionekani.
Alieleza kuwa alipomuuliza mlinzi wake, alisema kwamba kundi la watu
lilifika likiwa na mtu mmoja aliyejitambulisha kuwa Mkurugenzi wa Mji
wa Tarime na baada ya kujitambulisha, watu hao walianza kubomoa milango
na madirisha.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa Wilaya ya Tarime, Charles Mbushi,
alisema halmashauri haikutumia utaratibu wa kiungwana na kuita kitendo
hicho ni cha kinyama na kinapaswa kulaaniwa.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji huo, Venensi Mwamengo, alikiri
kubomolewa kwa vibanda hivyo na kuongeza kuwa wafanyabiashara hao
hawakufuata utaratibu.
Alisema waliamua kubomoa usiku kwa sababu wangebomoa mchana kugekuwa
na fujo hadi inawezekana watu wangepoteza maisha na kueleza kuwa hakuna
kitu chochote kilichopotea.
“Watu wa Tarime ni wababe sana, tungebomoa mchana kungetoa vurugu
kubwa, lakini pia tuliwapa barua na tuliwatangazia wote, lakini waligoma
kuondoka,” alisema
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment