Jaji mstaafu,Joseph Warioba.
Katibu wa CCM Wilaya ya Musoma Mjini, Jacob Nkomora, alitoa shutuma hizo katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na chama hicho mjini hapa juzi.
Mkutano huo uliofanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Kigera Manispaa ya Musoma, ulihudhuriwa na viongozi wa wilaya za mkoa wa Mara.
Nkomora alisema hatua ya Jaji Warioba kukubali kipengele cha rasimu ya Katiba mpya kinachoitaka nchi kuwa na serikali tatu, ni usaliti wa waziwazi kwa muasisi wa taifa ambaye mara na siku zote alipigania misingi ya umoja, mshikamano na upendo miongoni mwa Watanzania likiwamo suala la kulinda Muungano.
“Jaji Warioba amemsaliti marehemu Baba wa Taifa kwa kutaka kuvunja Muungano, kitendo ambacho ni cha usaliti kwa familia ya Nyerere na wana-Mara kwa ujumla na anatakiwa amuombe radhi mjane wa Mwalimu, Mama Maria Nyerere,” alisema.
Alisema Jaji Warioba katika nyadhifa zake mbalimbali alizowahi kuzitumikia enzi ya utumishi wake wa umma ikiwa ni pamoja na Uwaziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, aliapa kuilinda Katiba ya Jamhuri ya Muungano ikiwamo muundo wa serikali mbili.
Hata hivyo, alisema kwa hivi sasa kiapo hicho ameamua kukisigina na kushawishi Watanzania wakubali muundo wa serikali tatu, jambo ambalo lina nia mbovu ya kuuvunja Muungano uliodumu kwa takribani miaka 50 sasa.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Halmshauri Kuu ya CCM Wilaya ya Musoma Mjini, Vedastus Mathayo, aliwataka wananchi mkoani Mara kuwapuuza viongozi wa vyama vya upinzani hususani Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wanaotumia miradi ya serikali ya awamu ya nne kujipatia umaarufu kisiasa.
Badala yake aliwataka wawatake viongozi hao kuwaonyesha michango yao waliyotoa katika kuwaletea maendeleo.
Mathayo alisema ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kwangwa ya Mjini Musoma ambao ujenzi wake ulisimama kwa miaka kadhaa, ujenzi wa mradi mkubwa wa maji ulioko eneo la Bukanga sambamba na ujenzi wa barabara ya Nyerere kwa kiwango cha lami kutoka Musoma hadi Nyanguge mkoani Mwanza, utekelezaji wake unatokana na Ilani ya CCM ya mwaka 2010.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment