WAKATI
watu kumi wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuhusika na matukio
mfululizo ya mauaji wilayani Tarime, mkoani Mara, wakazi wa mji huo
wanaishi kwa mashaka na kushindwa kufanya shughuli zao za kila siku.
Mji wa Tarime hivi sasa haukaliki kutokana na msako mkali
unaoendeshwa na Jeshi la Polisi kila kona kwa lengo la kuwasaka watu
waliohusika na mauaji ya kinyama yaliyoutikisa mji huo kwa takribani
wiki tatu sasa.
Matukio hayo ya mauaji yamekuwa yakijirudia mara kwa mara na
kusababisha hofu kubwa miongoni mwa wakazi hao hadi kufikia hatua ya
kushindwa hata kufanya kazi zao za kila siku.
Katika kipindi cha siku tatu mfululizo, kundi la mauaji hayo ambalo
linadaiwa halizidi watu watano, limewaua kinyama watu wanane wasio na
hatia.
Wakizungumza kwa Nyakati tofauti na gazeti hili jana, baadhi ya
wananchi waliopoteza ndugu zao walisema kuna jambazi mmoja anayehusika
kupanga mauaji hayo.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime na Rorya, Justus Kamgisha,
aliliambia gazeti hili kuwa hadi sasa watu kumi wanashikiliwa na polisi
kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo.
Kamanda Kamgisha aliwataja waliouawa kuanzia Januari 27 hadi sasa
kuwa ni Marwa Nyitara, (30), Nkende Davidi, Matiko Yomami, Machungu
Nyamaheba, Sammy Magori, Marwa Nyaitara, Ericki Lucas, Chacha Magege na
mwingine aliyemtaja kwa jina moja la Mwasi.
Kwa mujibu wa Kamanda Kamgisha, uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa
muuaji huyo ambaye hajafahamika wala kukamatwa, ndiye kinara wa mipango
ya mauaji hayo na amekuwa akitumia silaha ambayo hadi leo haijafahamika
kwamba ni aina gani.
Ili kuongeza nguvu katika kuwasaka wauaji hao, alisema kuwa Mkuu wa
Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu ametuma timu maalumu kutoka
Makao Makuu ya Jeshi la Polisi nchini kuwasaka maharamia hao katika
maeneo ya Kenyamanyori, Rebu, Nkende, Mogabile, Kibumaye, Kitare na
Turwa, yote ya Tarafa ya Inchage.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment