CHAMA
Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mara kimeomba radhi kwa Chama cha Waandishi
wa Habari mkoani Mara (MRPC) kutokana na kitendo kinachodaiwa kufanywa
na wafuasi wa chama hicho, kwa kumpiga mwandishi wa habari wa gazeti la
Mwananchi, Christopher Maregesi, na kuahidi waliohusika watachukuliwa
hatua.
Mwenyekiti wa CCM mkoani Mara, Christopher Sanya, alisema chama hicho
kinamuomba radhi mwandishi huyo pamoja na waandishi wote mkoani Mara.
Sanya alisema chama hicho kitafanya uchunguzi na kuwachukulia hatua
wale wote watakaobainika kumshambulia mwandishi huyo wakati akitekeleza
wajibu wake.
Alisema chama hicho kinathamini na kutambua mchango wa mwandishi huyo
na waandishi wote kwa ujumla, hivyo kitendo kilichofanywa na watu
wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wao si cha kiungwana.
“Mimi nikiwa mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, kwa niaba ya chama
ninaomba radhi kwa kitendo alichofanyiwa mwandishi huyo wa habari na
watu wanaodaiwa kuwa ni makada wa chama, ninakemea, kwani si cha
kiungwana…tutafanya uchunguzi na wale watakaobainika watachukuliwa
hatua,” alisema.
Maregesi alishambuliwa na kupigwa Februari 8 mwaka huu na watu
wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa CCM katika eneo la chama hicho mjini
Bunda, muda mfupi baada ya mkutano wa kampeni wa kumnadi mgombea udiwani
katika Kata ya Nyasura, Alexander Mwikwabe kumalizika.
Chanzo;Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment