IDARA ya elimu katika wilaya ya Bunda, mkoani Mara, inakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwemo ya upungufu wa walimu kwa shule za msingi, kutokana na idadi kubwa ya walimu kustaafu kila mwaka.
Afisa elimu wa shule za msingi wilayani Bunda, Bw. Jeshi Lupembe ameyasema hayo kwenye kikao cha kawaida cha baraza la madiwani cha robo ya mwaka, katika ukumbi wa halmashauri mjini Bunda.
Bw. Lupembe amesema kuwa idara ya elimu wilayani hapa, pamoja na kuwa na changamoto ya miundombinu,pia kuna upungufu mkubwa wa walimu kwa shule za msingi kwani wengi wao wanastaafu kila mwaka.
Amefafanua kuwa mwaka 2013/2014 jumla ya walimu 80 watastafu na kuongeza kuwa halmashauri ya wilaya hiyo mahitaji ya walimu ni 1902, waliopo ni 1634 na upungufu ni walimu 268.
Ameiomba serikali kuliona hilo na kuwaletea walimu ili kukabiliana na changamoto hiyo.
Aidha amesema kuwa pamoja na kuhamia wilayani hapa hivi karibuni akitokea mkoani Kilimanjaro, lengo lake kuu ni kuinua kiwango cha elimu katika wilaya hiyo.
Ameongeza kuwa yuko tayari kushirikiana na madiwani hao kwa ajili kuboresha elimu ili maendeleo yake yaweze kuwa endelevu, ikiwa ni pamoja na kuinua kiwango cha taaluma.
Akizungumzia mradi wa chakula mashuleni ulioletwa na shirika la PCI, amesema kuwa mradi huo umeonyesha mafanikio makubwa, kwani mahudhurio kwa wanafunzi yamepanda sana tofauti na awali.
Wakati huo huo, diwani wa kata ya Salama (CCM) mheshimiwa Said Kuvyenda, amesema kuwa mradi wa PCI umekuwa mkombozi kwa shule za kata yake na kuongeza kwa wananchi wameupokea mradi huo kwa furaha kubwa.
Bw. Kuvyenda amesema kuwa yeye ni mmoja wapo aliyepigania mradi huo ili uweze kufikishwa kwnenye shule za kata yake.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment