KUTOKANA na idadi kubwa ya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi ambao wamekatisha matibabu yao na kutokomea kusikojulikana, idara ya afya wilayani Bunda mkoani Mara, kupitia kitengo chake cha ukimwi, imesema kuwa itawasaka watu hao ili waweze kuendelea na matibabu yao kama kawaida.
Mratibu wa ukimwi wilayani Bunda, Dk. Nelson Malisa, ameyasema hayo jana kwenye semina ya kuwajengea uwezo madiwani wa halmashauri hiyo juu ya suala zima la kuwepo makundi maalumu katika jamii ambayo ndiyo yanaoathirika zaidi na virusi vya ukimwi.
Dk. Malisa amesema kuwa walipoanza kutoa huduma ya matibabu kwa watu waishio na virusi vya ukimwi, kulikuwa na wanaume 4,514 na wanawake 4,933, lakini sasa idadi hiyo imepungua ambapo wanaume ni 1,185 na wanawake ni 2,654 tu.
Amefafanua kuwa wagonjwa waliohama ni 1,990, waliokufa ni 603 na ambao wamepotea na hawajulikani walipo ni 715 tu.
Amesema kuwa kutokana na watu hao kutojulikana walipo, sasa watawatafuta kupitia kwa wahudumu wa afya ya jamii majumbani, ili waweze kuendelea na dozi zao kama kawaida.
Mraribu wa shughuli za ukimwi katika halmashauri ya wilaya ya Bunda, Bi. Mariam Mbaraka, amesema kuwa makundi maalumu yamekuwa yakiambukizwa virusi vya ukimwi kutokna na sababu mbalimbali.
Bi. Mariam amezitaja sababu hizo kuwa ni pamoja na kujahamiana, ngono zisizo salama na wengine kufanya tendo hilo kinyume cha maumbile.
Aidha, amesema kuwa wilaya ya Bunda inakabliwa na kuwepo kwa wanaume kujahamiana wenyewe kwa wenyewe (mashoga) ambapo wengi wao inadaiwa kuwa ni vijana ambao wamejiingiza katika hali hiyo.
Akifunga semina hiyo mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Bunda, Bw. Joseph Malimbe, amewataka madiwani hao kuifikisha elimu waliyoipata kwa jamii inayowazunguka, ikiwa ni pamoja na kuwataka wazazi kufuatilia miendendo ya watoto wao wakiwemo wanafunzi.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment