WAFUGAJI wa mifugo wa vijiji vya Mangucha, Kegonga, Masanga na
Gibaso, kata za Nyarukoba, Gorong’a na Nyanungu wamelazimika kuingiza
mifugo yao katika Bonde la Nyanungu lililomo ndani ya Hifadhi ya Mbuga
ya Taifa ya Serengeti kinyume cha sheria baada ya mabwawa
waliyochimbiwa na SENAPA kukosa maji.
Wakielezea adha hiyo, madiwani Mustapha Masian (Nyarukoba), Magarya
Wambura (Gorong’a) na Mang’enyi Ryoba (Nyanungu), walisema ukosefu wa
maji kutokana na kukauka kwa mabwawa hayo, umesababisha kuuawa kwa
mifugo kwa kupigwa risasi na askari wa wanyama pori kutokana na wafugaji
kulazimika kuingiza mifugo yao katika hifadhi hiyo.
Madiwani hao walisema ukosefu huo wa maji umesababisha pia kukamatwa
na kufikishwa mahakamani kwa baadhi ya wafugaji na kupigwa faini baada
ya kukutwa wakichunga katika bonde hilo.
“SENAPA walichimba mabwawa ya kunyweshea mifugo mwaka 2006/2007
katika vijiji vya Mangucha na Masanga ambayo tangu mwaka huo hayajatoa
maji kutokana na kuchimbwa vibaya, na kwamba SENAPA hawakuweza kurudi
tena kufanya marekebisho hayo ili yaweze kutoa maji kuondoa kero ya
maji ya mifugo kuingia hifadhini,” alisema mmoja wa madiwani hao.
Walisema wananchi wameshindwa kuendeleza miradi mingine ya shule
baada ya kuendeshwa ujenzi wake wa vyumba vya madarasa vinne vya kila
shule za msingi za Kegonga na Mangucha mwaka 2001/2002 na SENAPA
kutokana na vijiji hivyo ardhi zake kuingia katika hifadhi hiyo.
Watendaji wa kata hizo, Gorong’a (Hezron Makaranga), Nyanungu
(Deodatus Waikama) na Nyarukoba (Lucas Kichogo), waliliambia gazeti
hili kuwa walitekeleza maazimio ya vikao vyao vya kata vya kamati za
maendeleo za kata (WDC) vilivyoketi kwa kuwaandikia barua SENAPA
kutekeleza maazimio ya kukutana kila baada ya miezi mitatu.
Hata hivyo, watendaji hao wamesema uongozi wa SENAPA ulishindwa
kuitikia vikao hivyo ikiwa ni njia ya kuweka mahusiano baina yao na
wananchi kujadili na kuamua utekelezaji wake.
“Kwa mujibu wa rejea ya vikao vyetu ya ujirani mwema, na kile
kilichohudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Tuppa, cha Julai 22,
2013 tulichoketi Kijiji cha Kegonga kuwa tuwe tunakutana mara baada ya
miezi mitatu ama dharura, SENAPA hawajatekeleza hilo,” alisema mtendaji
wa Kata ya Nyanungu, Waikama.
Waikama alisema kuwa wamechukua hatua ya kumjulisha Mkuu wa Wilaya,
John Henjewele na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Tuppa, ambao walimtaka
muhifadhi mkuu wa SENAPA, William Mwakilema kutekeleza maazimio ya
vikao vya kata hizo.
Ukosefu wa malisho kwa wafugaji wa mifugo katika vijiji hivyo na
malambo ya kunyweshea mifugo yao kushindwa kutatuliwa na SENAPA
kumeibua matukio ya ukiukaji wa sheria na kuzua uhasama mkubwa baina ya
askari wa wanyama pori na wananchi wa vijiji hivyo, hasa baada ya
kushindwa kutatuliwa changamoto zilizopo kwa njia ya vikao vya pamoja.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment