Home » » Mdunguaji wa Tarime afariki dunia

Mdunguaji wa Tarime afariki dunia

Kamanda wa Polisi Kanda ya Tarime/ Rorya, Justus Kamugisha.
 
Mtuhumiwa wa mauaji na unyang’anyi wilayani Tarime mkoani Mara, aliyekuwa akitumia majina matatu ya Charles  Range Kichune, Josephat Chacha, Charles Joseph Msongo (38) aliyekuwa akihojiwa na Polisi, amefariki katika Hospitali ya wilaya wakati akipatiwa matibabu.
Kamanda wa Polisi Kanda ya Tarime/ Rorya, Justus Kamugisha, alisema mtuhumiwa huyo alifariki usiku wa kuamkia jana wakati akitibiwa ugonjwa wa pumu na kwamba baada ya kugunduliwa kuwa na ugonjwa huo, alipelekwa hospitalini. Kamanda Kamugisha alisema mwili umehifadhiwa  kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi.

Alisema kabla ya kufariki, mtuhumiwa  alikiri kuhusika katika mauaji ya watu tisa katika kata za Binagi, Turwa na Kitare katika Vijiji vya Mogabiri, Kenyamanyori, Nkende na Rebu.

Kamanda huyo alisema Range Kichune alikamatwa Februari 6, mwaka huu  mkoani Tanga baada ya Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na raia wema kufuatilia mtandao wake na kuwa ilidaiwa baada ya mauaji ya hao alikodi pikipiki kutoka kijijini kwake Kenyamanyori  hadi Musoma na kuhifadhi bunduki SMG na risasi kadhaa kwa mshirika wake mkuu.

Alipokamatwa alimtaja Marwa Keryoba kuwa mshirika wake na kuwa alihifadhi silaha hiyo kwake na Marwa aliuawa Februa 7, mwaka huu Musoma wakati akirushiana risasi na polisi alipotakiwa kujisalimisha.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa