Home » » Muuaji wa raia Tarime akamatwa

Muuaji wa raia Tarime akamatwa

MTU anayedaiwa kuwa ni jambazi anayeua raia wasiokuwa na hatia katika vijiji mbalimbali Wilaya ya Tarime mkoani Mara, amekamatwa. Muuaji huyo anayetembea na bunduki ya SMG, alikamatwa juzi katika Mkoa wa Tanga, wakati akitoroka baada ya kuua watu 10 wasiokuwa na hatia mwishoni mwa mwezi Januari.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime /Rorya, Justus Kamugisha alisema mtu huyo alikuwa akitumia majina mengi kwa ajili ya kumfanya asitambulike haraka na kwa urahisi.

Kwa mujibu wa Kamanda Kamugisha, mtu huyo amekuwa akijitambulisha kwa jina la Charles Range Kichune, Josephat Chacha, Charles Joseph Msong’o (38) mkazi wa Kijiji cha Kenyamanyori Kata ya Turwa wilayani Tarime.

“Mtu huyu amekamatwa mkoani Tanga Februari 6 majira ya saa 1:30 jioni. Hata hivyo hakuwa na silaha yoyote ndani ya begi lake la nguo. Takribani raia 10 wameaga dunia kwa kuuawa na mtu huyu, ambaye amekiri kuhusika na matukio hayo yote.
Chanzo;Mtanzania 


“Baada ya kumweka chini ya ulinzi na kuanza kumhoji, ndipo tukagundua kuwa si yeye peke yake anayefanya matukio haya bali wako wengi japokuwa aliyekuwa akifahamika ni yeye tu,” alisema.

Kamanda Kamugisha alisema, alipohojiwa zaidi mtu huyo alieleza ilipo silaha anayoitumia na kuwaomba askari kuwapeleka alikokuwa ameificha.

“Polisi mkoani Tanga waliondoka hadi mkoani Mara, ambapo aliwafikisha kwa jambazi mwenzake aliyemwachia baada ya kuona kuwa Jeshi la Polisi limeanza kumtafuta.

“Aliwapeleka maofisa wa Jeshi la Polisi hadi Kijiji cha Bweri Musoma mjini, kwa mwenzake aliyemtaja kwa jina la Marwa Keryoba au Alex anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 30 na 38, ambaye ni mkazi wa Sirari akiishi Musoma.

“Wakati polisi wanaingia kwa Keryoba, aliwasikia na kutoka nje akiwa amevaa koti refu jeusi kisha kulitupa chini kwa lengo la kupoteza mwonekano wake.

“Hata hivyo polisi walipiga risasi juu kumtaka ajisalimishe, japo alianza mashambulizi kuwashambulia maaskari hao.

“Askari walimuua Keryoba kwa kumpiga risasi baada ya kukaidi amri ya Jeshi la Polisi, lililomtaka ajisalimishe, kwa vile alikuwa amebeba silaha ya SMG iliyokatwa kitako na mtutu huku imefutika namba,” alisema Kamugisha na kuongeza:

“Baada ya kumpekua walimkuta akiwa na vitu vifuatavyo, SMG iliyofungwa tochi kwenye mtutu, magazine moja yenye risasi kumi na kwenye nyumba aliyokuwa anaishi marehemu zilipatikana simu mbili za mkononi.

“Vitu vingine ni CD 21 za picha mbalimbali, deki moja, viatu pea mbili aina ya buti, tochi mbili na mpira wa baiskeli pamoja na bidhaa mbalimbali za dukani,” alisema.

Kamugisha aliwaomba wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kurahisisha utendaji wa kazi wa chombo hiki chenye dhamana ya kulinda usalama wa raia na mali zao.
Chanzo;Mtanzania   

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa