SIKU
moja baada ya kukamatwa, kupigwa na kisha kuporwa vifaa vyake vya kazi,
mwandishi wa habari wa Kampuni ya Mwananchi wilayani Bunda, Christopher
Malegesi, na kiongozi mmoja wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa, Chama
cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara (MRPC), kimetangaza kugoma kuandika
habari za chama hicho.
Mwenyekiti wa chama hicho, Emanuel Bwimbo, aliiambia Tanzania Daima
kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya kuona kitendo hicho kimefanyika kwa
makusudi.
“Kitendo alichofanyiwa ni cha kinyama na kinakiuka Katiba ya Jamhuri
ya Muungano Ibara ya 18. Sisi kama chama pia tumeamua kamwe hatutaandika
habari za CCM, bali tutaandika maovu yao kama yakijitokeza.
“Kamwe hatutaenda katika ziara zao na wala mikutano yao maana wao ni mabingwa wa kupiga,” alisema Bwimbo.
Alisema kwa muda mrefu waandishi wa habari wamekuwa wakionewa na
kupigwa katika mikutano ya CCM huku serikali ikifumbia macho, jambo
ambalo limekuwa likiweka chuki kati ya waandishi na chama hicho.
Bwimbo aliwataka watendaji wa serikali likiwemo Jeshi la Polisi na
CCM kutambua kuwa taaluma ya habari inatambulika ulimwengu mzima, na
kwamba kama CCM wanataka kufanya mchezo basi wataona nguvu ya kalamu.
Awali akizungumzia tukio la kupigwa kwa mwandishi huyo, Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Mara, Ferinandi Mtui, pamoja na kulaani kitendo hicho
aliahidi kusimamia suala hilo na kuhakikisha waliofanya hivyo
wanafikishwa mahakamani.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment