WAZIRI
wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Bw. Stephen Wassira,
amemshukia Mbunge wa Arusha Mjini, Bw. Godbless Lema na kudai ndiye
chanzo cha vurugu ambazo zinatokea katika mji huo na kuzorotesha soko la
utalii kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Bw. Wassira aliyasema hayo
juzi katika mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani, Kata ya
Nyasura, Jimbo la Bunda, mkoani Mara.
Alisema awali Mji wa Arusha
ulisifika kwa kuwa na amani lakini baada ya Uchaguzi Mkuu 2010, Mji huo
umepoteza sifa ya kutembelewa na wageni mbalimbali kutokana na siasa za
fujo, vurugu na mapigano.
"Wananchi wanapandikizwa chuki dhidi ya
Serikali yao, wanasiasa mfano wa akina Lema ndio wanaovuruga amani ya
nchi yetu hivyo wakazi wa hapa Nyasura epukeni watu kama hawa," alisema
Bw. Wassira.
Alisema hivi sasa kuna njama zinazopangwa na CHADEMA
ili vijana wao wakafanye vurugu katika uchaguzi wa udiwani ili kuwatia
hofu wanawake na wazee wasijitokeze kumchagua diwani wanayemtaka
Februari 9 mwaka huu.
Aliongeza kuwa, vyombo vya usalama vimejipanga
kudhibiti fujo hizo na kuwatoa hofu wananchi akiwataka wajitokeze kwa
wingi kupiga kura siku hiyo.
"Naomba wananchi mfanye tathmini juu ya
siasa zinazofanywa na viongozi wa CHADEMA kwa kulazimisha wananchi
kuvunja sheria za nchi, mwanasiasa mzuri anapaswa kutumia nguvu ya
ushawishi kwa kujenga hoja si kuchochea chuki, ugomvi na matusi kwa
wananchi," alisema.
Alimtuhumu Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Bw.
Freeman Mbowe na kudai anawapotosha wananchi ili waunge mkono Serikali
tatu wakati Katiba Mpya ni ya Watanzania wote.
"Lazima tujadili
mfumo wa Muungano wa Serikali mbili kwa kuzingatia maslahi ya Taifa
kihistoria, kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiusalama lakini si kwa
maslahi ya chama fulani, kama tutaona mfumo wa Serikali tatu haifai kwa
nchi yetu ni vyema tukaachana nao," alisisitiza Bw. Wassira.
Alisema
Rasimu ya Pili ya Katiba itajadiliwa katika Bunge Maalumu la Katiba na
baadaye wananchi watapewa fursa ya kutoa maoni yao na kuwataka wananchi,
wajihadhari sana na mfumo wa Serikali tatu.
Operesheni ya CHADEMA
Akizungumzia
Operesheni ya Mabadiliko Pamoja Daima inayofanywa na CHADEMA, Bw.
Wassira alisema imelenga kuokoa mpasuko wa ndani ya chama chao ambao
umeikumba kambi ya Bw. Zitto Kabwe na Bw. Mbowe.
Bw. Wassira
alikwenda mbali zaidi na kudai kuwa, CHADEMA si chama cha kuwatetea
wananchi maskini bali wanatumia umaskini wa Watanzania kutaka kuingia
Ikulu jambo ambalo linapingwa na wananchi wengi wanaotambua dhamira
hiyo.
"Mwanzilishi wa CHADEMA ni Edwin Mtei aliyetofautiana na
Hayati Mwalimu Julius Nyerere, wakati Mwalimu anatetea maskini kwa siasa
ya ujamaa na kujitegemea, Mtei alitetea ubepari hivyo Mwalimu
akamfukuza serikalini.
"Jambo hili lilimkasirisha Mzee Mtei akaamua
kupambana na TANU na hatimaye CCM, leo wanatudanganya kwamba wanawatetea
Watanzania maskini," alisema Bw. Wassira.
Alitumia fursa hiyo
kumnadi mgombea wa CCM, katika kata hiyo, Bw. Alexander Mwikwabe
akiwataka wananchi watumie vizuri kura zao kumchagua mgombea wao
Chanzo;Majira
0 comments:
Post a Comment