Home » » Bunda yapata walimu wapya 223

Bunda yapata walimu wapya 223

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, imeipatia Wilaya ya Bunda jumla ya walimu wapya 223, wakiwemo wa sekondari 137 na shule za msingi 86.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Simon Mayeye, alieleza hayo jana wakati wa hafla ya kupokea msaada wa vifaa vya kompyuta vilivyotolewa na Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF).
Vifaa hivyo vyenye thamani ya sh milioni 5.2, vimetolewa na PSPF kwa halmashauri hiyo baada ya kompyuta iliyokuwepo kwa ajili ya kuingiza majina ya watumishi wa halmashauri kupigwa na radi na kuungua.
Mayeye alisema walimu hao wameajiriwa na serikali katika ajira mpya na kwamba tayari wamekwishaanza kupokewa katika halmashauri yake.
Alisema hadi jana walikuwa wamepokewa walimu 48 wa sekondari na 36 wa shule za msingi na kuingizwa kwenye kumbukumbu za halmashauri hiyo, ikiwa ni pamoja na kuanza zoezi la kuwagawa kwenye vituo vyao vya kazi.
Aidha, alisema wilaya hiyo inakabiliwa na upungufu mkubwa wa walimu, kutokana na idadi kubwa ya walimu kustaafu kwa mujibu wa sheria.
Akikabidhi msaada huo, Ofisa Mfawidhi wa PSPF mkoani Mara, Sudi Hamza, alisema wametoa vifaa hivyo baada ya halmashauri hiyo kupeleka maombi kutokana na kompyuta iliyokuwepo kupigwa na radi.
Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa