Home » » MJI WA KIBARA WAKUMBWA NA TAHARUKI

MJI WA KIBARA WAKUMBWA NA TAHARUKI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
 
WAKAZI wa mji mdogo wa Kibara, wilayani Bunda wametahamaki na kuingiwa na hofu, baada ya kuwepo taarifa kuwa mtoto aliyepotea katika mazingira ya kutatanisha, mwili wake umepatikana katika kijiji jirani ukiwa umechunwa ngozi.
Kutokana na hali hiyo, wananchi hao wakiwemo waendesha Bodaboda, waliandamana na kwenda katika eneo la tukio, katika kijiji jirani cha Negongo, ambako ilidaiwa kuwa kuna mwili wa mtoto huyo.
Baada ya wananchi hao waliokuwa na jazba, wengi wao wakiwa wanawake kufika katika eneo hilo, hawakukuta kitu chochote, na ndipo ikabainika kuwa habari hizo zilikuwa ni za uzushi mtupu.
Ilidaiwa na wazazi wa mtoto huyo Selemani Baraka (4) kuwa alipotea Aprili 3 mwaka huu, saa 5:00 asubuhi akiwa anacheza katika enao la nyumbani kwao katika mazingira ya kutatanisha.
Ofisa mtendaji wa kijiji cha Kibara kilichoko katika mji mdogo wa Kibara, Bagaire Masatu, alisema mtoto huyo alipotea katika mazingira ya kutatanisha na kwamba tayari tukio hilo limeripotiwa katika kituo cha polisi Kibara.
Masatu alisema pamoja na juhudi za kutafuta mtoto huyo kufanyika hadi jana bado alikuwa hajapatikana.
“Baada ya ofisi hii kupata taarifa ya kupotea kwa mtoto huyo, tulitoa taarifa polisi na kupiga kengele kwa ajili ya kuanza kumtafuta, lakini hadi leo (jana) bado hatujampata,” alisema ofisa mtendaji huyo.
Aidha aliwaomba wasamaria wema watakaomuona mtoto huyo, watoe taarifa kwenye kituo chochote cha polisi au ofisi yoyote ya Serikali. Naye mzazi wa mtoto huyo Baraka Baraka, alisema anawaomba wasamaria popote watakapomuona mtoto huyo watoe taarifa kituo cha polisi Kibara.
Chanzo;Habari Leo

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa